1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kashfa ya ngono yazusha mtafaruku katika serikali ya mseto

18 Februari 2014

Uchunguzi unaofanywa katika kashfa inayomkabili mwanasiasa wa chama cha SPD Sebastian Edathy ya picha za ngono za watoto umeingia katika hatua ya mapambano.

https://p.dw.com/p/1BAn1
Sigmar Gabriel, Angela Merkel, Horst Seehofer
Kutoka kushoto ni Sigmar Gabriel,(SPD) Angela Merkel (CDU) na Horst Seehofer(CSU)Picha: picture-alliance/dpa

Mwanasiasa huyo alitoa taarifa kwa polisi kuwa Laptop yake ya kazini imeibiwa.

Wachunguzi mjini Hannover hata hivyo hawakujua chochote kuhusu taarifa hiyo kwa siku nzima.

Katika uchunguzi wa kashfa hiyo hata hivyo dhidi ya mwanasiasa huyo wa chama cha SPD kila wakati sasa kunapatikana kitu kipya.

Sebastian Edathy Porträt
Anayechunguzwa Sebastian Edathy,(SPD)Picha: picture-alliance/dpa

Sebastian Edathy kwa hiyo alitoa taarifa kwa polisi wa bunge katika wiki kadha zilizopita kuwa Laptop yake ya kazi imeibiwa , siku kadha baada ya kujiuzulu wadhifa wake na waendesha mashtaka mjini Hannover kupekua nyumbani kwake pamoja na ofisi yake.

Hayo yamethibitishwa na msemaji wa bunge. Hata hivyo polisi waliokuwa wakifanya uchunguzi mjini Hannover hawakufahamu lolote kuhusu taarifa hiyo ya wizi kwa muda wa siku nzima.

Kansela wa Ujerumani na mwenyekiti wa chama cha CDU Angela Merkel , mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel na mkuu wa chama cha CSU Horst Seehofer watakutana jioni ya leo kuzungumzia suala hilo.

Serikali ya mseto yakabiliwa na maswali kadha

Serikali ya mseto inapaswa kutoa majibu kwa maswali kadha. Mkuu wa wabunge wa chama cha SPD katika bunge la Ujerumani Thomas Oppermann anakabiliwa na ukosoaji mkubwa. Aliweka wazi wiki iliyopita kwamba waziri wa zamani wa mambo ya ndani Hans-Peter Friedrich kutoka chama cha CSU amemweleza mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel kuwa jina la Edathy limejitokeza kwa wachunguzi wa nje.

Hans-Peter Friedrich gibt seinen Rücktritt bekannt
Waziri Hans-Peter Friedrich aliyejiuzuluPicha: picture-alliance/dpa

Friedrich alilazimika kujizulu wadhifa wake siku ya Ijumaa akiwa kama waziri wa kilimo na chakula wa Ujerumani. Ameshutumiwa kuwa amekuwa msaliti kwa kufichua siri.

Hata hivyo kujiuzulu kwa waziri Friedrich kumezusha hali ya kulipiza kisasi dhidi ya chama cha SPD , chama ambacho kimo ndani ya serikali ya mseto inayoongozwa na kansela Angela Merkel ya kile kinachofahamika kama "Muungano mkuu". Jana Jumatatu mwanasiasa wa chama cha SPD Hannelore Kraft amesema kuwa anatambua hasira ya chama cha CSU.

Sigmar Gabriel PK 17.02.2014
Sigmar Gabriel kiongozi wa chama cha SPDPicha: picture-alliance/dpa

"Natambua kwamba chama cha CSU hakijafurahishwa na kujiuzulu kwa waziri Friedrich, lakini hakuna sababu ya kulipiza kisasi, jicho kwa jicho , jino kwa jino."

Hali ya hewa imechafuka

Ni dhahiri basi kuanguka kwa waziri huyo kutoka chama cha kihafidhina cha CSU kumechafua hali ya hewa katika serikali hiyo mpya ya muungano, lakini viongozi wa vyama wameweka wazi jana Jumatatu kuwa hawataruhusu hali hiyo kuiangusha serikali katika wakati huu tete wa kuongoza mpango wa mageuzi.

Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanatarajia kuwa serikali hiyo ya mseto , ambayo ina wingi mkubwa bungeni, itarejea katika shughuli zake za kawaida baada ya muda mfupi wa kupigana vikumbo kati ya wahafidhina wakiongozwa na Merkel , chama ndugu cha jimbo la Bavaria kinachoongozwa na Horst Seehofer na chama cha SPD kinachoongozwa na Sigmar Gabriel.

Christian Schmidt und Horst Seehofer Archiv 2013
Horst Seehofer kiongozi wa chama cha CSU(kulia)Picha: picture-alliance/dpa

"Kashfa hii inaleta madhara kwa hali katika serikali ya mseto pamoja na heba yake, na nafikiri itachukua muda kabla ya kurejea katika hali ya kawaida ya kufanya kazi," amesema Carsten Koschmieder, mtaalamu wa sayansi ya kisiasa katika chuo kikuu huria cha mjini Berlin.

"Lakini Merkel , Seehofer na Gabriel wanatambua kuwa hakuna mbadala. Merkel hana mshirika mwingine wa kuunda serikali anayesubiri, na wote wanafahamu huenda wakaporomoka katika kuungwa mkono iwapo kutafanyika uchaguzi mpya. Kwa hiyo licha ya mapambano, muungano mkuu utaendelea.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri : Hamidou Oummilkheir