1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu Mkuu Ban kuzuru Bara la Afrika

P.Martin - (AFP)19 Februari 2009

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ataanza ziara ya mataifa matano ya Afrika mapema wiki ijayo,zikiwemo ziara zake za kwanza rasmi nchini Afrika Kusini na Tanzania.

https://p.dw.com/p/GxcI
ARCHIV - UN-Generalsekretär Ban ARCHIV - UN-Generalsekretär Ban Ki Moon (Archivfoto vom 12.12.008) hat erneut zu einem sofortigen Ende der Gewalt und der Militäroperationen im Gazastreifen aufgerufen. In einer Mitteilung der Vereinten Nationen aus der Nacht zum Montag (29.12.2008) hieß es, Ban bedauere, dass die Gewalt weitergehe. Er habe mit Mitgliedern des Nahost-Quartetts und dem amtierenden israelischen Ministerpräsidenten Olmert, Palästinenserpräsident Abbas, dem ägyptischen Präsidenten Mubarak, dem syrischen Präsidenten al-Assad sowie dem Generalsekretär der Arabischen Liga, Moussa, gesprochen. Im Nahost-Quartett sind USA, EU, Russland und UN vertreten. EPA/SALVATORE DI NOLFI +++(c) dpa - Bildfunk+++ (
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.Picha: picture-alliance/ dpa

Katibu Mkuu Ban Ki-moon atazizuru pia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Rwanda na Misri. Kwa mujibu wa msaidizi wa msemaji wake Marie Okabe, kwanza Ban Ki-moon ataelekea Afrika Kusini kwa mazungumzo na Rais Kgalema Motlanthe pamoja na mawaziri wake wa fedha na mazingira. Anatarajiwa pia kukutana na rais wa zamani Nelson Mandela.

Kutoka Afrika Kusini ataelekea mashariki mwa bara hilo nchini Tanzania. Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa,mbali na kukutana na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete,atazungumza pia na mabalozi na wasomi mjini Dar-es-salaam. Kadhalika atafungua ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Zanzibar itakayokuwa na ofisi za mashirika yote ya Umoja wa Mataifa.Ban anapanga pia kwenda kaskazini mwa Tanzania kuitembelea Mahakama ya Kimataifa kuhusu Rwanda mjini Arusha.

Kituo cha tatu cha ziara yake kitakua ni katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Atakutana na Rais Joseph Kabila na kuzungumza pia na wabunge na wajumbe wa jumuiya za kiraia nchini humo. Baadae ataelekea mashariki mwa Kongo mjini Bukavu,ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu ya Kusini. Huko atatembelea hospitali ya "Panzi" inayowahudumia wahanga waliobakwa wakati wa vita na machafuko katika eneo hilo. Atakapokuwa mjini Goma,baadae atakutana na wajumbe wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa-MONUC- pamoja na viongozi wa eneo hilo na pia kuizuru kambi ya waliopoteza makaazi yao kutokana na mgogoro mashariki mwa Kongo.Umoja wa Mataifa una wanajeshi 17.000 nchini Kongo, idadi kubwa kabisa ya wanajeshi wa kulinda amani wa umoja huo katika eneo la mgogoro duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban-Ki-moon ataelekea baadae mjini Kigali nchini Rwanda kwa mazungumzo na Rais Paul Kagame.Atakamilisha ziara yake katika mji wa Sharm-El-Sheikh nchini Misri,ambako tarehe 2 Machi atahudhuria mkutano wa kimataifa wenye lengo la kuinua uchumi wa Palestina na kugharimia ujenzi mpya katika Ukanda wa Gaza, baada ya kuharibiwa vibaya kutokana na hujuma za majeshi ya Israel za siku 22 mwezi uliopita. Mkutano huo utasimamiwa kwa pamoja na Misri na Norway.

Kwa mujibu wa tangazo la Umoja wa Mataifa, mbali na kusema kuwa ziara hiyo barani Afrika itaanza mapema mwezi ujao,tarehe hasa za kuwasili katika nchi nyengine nne mbali ya Misri,hazijatangazwa.