1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu Mkuu wa UN,Ban Ki-moon alitetea Shirika la FAO.

6 Mei 2008

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amelitetea Shirika la Kilimo na chakula la Umoja huo-FAO dhidi ya tuhumu zilizotolewa na Rais wa Senegal.

https://p.dw.com/p/DuOo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon Akizungumza katika Mkutano wa hali ya hewa uliofanyika Dec. 11, 2007 nchini Indonesia.Picha: AP

Rais Abdoulaye Wade, alilishutumu shirika hilo kuwa limeshindwa kushughulikia changamoto za ongezeko la njaa ulimwenguni.

Shutuma hizi kali zilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Rais Wade wa Senegal, ambaye alilielezea Shirika la Kimataifa la Kilimo na Chakula kuwa halina kazi yoyote linayoifanya zaidi ya kupoteza fedha na kwamba fedha nyingi limekuwa likizitumia kwenye miradi midogo ambayo haikuleta mafanikio yoyote.

Akizungumza na waandishi wa habari, Ban Ki-moon, alisema kuwa kwa kuzingatia mvutano na ugumu wa hali ilivyo, anaweza kuelewa na kusikitishwa na jinsi ambavyo viongozi wengi wa Afrika wanavyochanganyikiwa akiwemo pia Rais Wade wa Senegal.

Lakini alisema angependa kusisitiza kuwa tangu kuanzishwa kwa FAO, mwaka 1945, Shirika hilo limekuwa likiendesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya kusaidia kuendeleza uzalishaji na kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao hususani ya chakula.

Mbali na shughuli hizo pia FAO, imekuwa ikijitahidi kusambaza misaada ya kibinadamu kwa watu wengi zaidi walioathirika na matatizo ya chakula.

Rais Abdoulaye Wade, alisema Shirika la FAO, ambalo linaongozwa na Raia kutoka Senegal Jacques Diouf ambaye rais Wade amesema alisaidia kuchaguliwa kwake, linapaswa kuunganishwa na Shirika jingine lenye makao yake makuu Roma, la Maendeleo ya kilimo-IFAD:

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kutengeneza kitu kimoja kinachoshughulikia masuala ya kilimo.Kwa sasa baadhi ya kazi zinazofanywa na Mashirika hayo mawili ya Kimataifa zinalingana.

Rais Wade alisema endapo Chombo kama hicho kitatengenezwa basi shughuli zake zielekezwe katika nchi za Afrika badala ya Nchi za Magharibi.

Ama kwa upande mwingine Benki ya Dunia ambayo ni kitu kimoja katika Umoja wa Mataifa, inatajwa kuwa pia inapaswa kulaumiwa kutokana na hali ya sasa ya mgogoro wa chakula kwa kushindwa kusaidia katika utafiti wa masuala ya kilimo kwa kipindi cha miaka kadhaa sasa.

Akiulizwa juu ya kushindwa huko, Rais wa Benki Kuu ya Dunia, Robert Zoelliki, alikubali kuwa ni kweli Taasisi hiyo imeshindwa lakini pia akasema kushindwa kwake kulichangiwa na matatizo ya Serikali za nchi husika.

Bwana Zoellick, alisema Benki ya Dunia pamoja na Serikali za nchi zimewekeza kiasi kidogo zaidi katika kilimo na kwamba kama Benki ya Dunia wanautaratibu wao wa kuweza kuzifikia nchi husika, ambapo nchi hizo zinaweza kuamua ni kitu gani zinaweza kukishughulikia.

Amesema zaidi walikuwa wakishughulikia masuala kama magonjwa ya UKIMWI, Malaria na miradi mingine.

Hata hivyo rais huyo wa Benki ya Dunia, amesema hadhani kwamba kitendo cha kuanza kuorodhesha matatizo na majukumu kitaweza kusaidia, lakini swali kubwa zaidi ni kwamba je kweli kuna tatizo la mahitaji,na jinsi gani wataweza kuyashughulikia, na hilo ndilo jambo ambalo amekuwa akiliangalia muda mfupi tu baada ya kushika nafasi hiyo.

Shirika la FAO, linajiandaa kwa Mkutano wa Viongozi duniani utakaofanyika mwezi ujao.

Kwa mara ya kwanza shirika hilo liliandaa Mkutano mkubwa wa Dunia juu ya chakula mjini Roma mwaka 1974, ambao ulitoa tamko kuwa kila mwanamume, mwanamke na mtoto ana haki zote za msingi za kutokabiliwa na njaa pamoja na utapiamlo kwa lengo la kuendeleza maisha yao.

Mwaka 1976, FAO iliandaa Mkutano mwingine kama huo wa siku tano ambao uliendeleza matamko ya mkutano wa mwaka 1974.

Malengo yote ya mikutano hiyo ni kumaliza tatizo la njaa, uhifadhi wa chakula na kupunguza utapiamlo katika kipindi cha muongo mmoja.Hata hivyo mpaka sasa malenggo hayo hayajafikiwa.