1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya huenda ikakosa michezo ya Olimpiki

19 Februari 2016

Wakuu wa riadha nchini Kenya wamepuuza tahadhari kuwa timu yake huenda ikapigwa marufuku kushiriki katika mashindano ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro, Brazil mwezi Agosti

https://p.dw.com/p/1HylB
China Leichtathletik WM in Peking - Nicholas Bett
Picha: Getty Images/C. Petersen

Hiyo ni ikiwa chama cha riadha nchini humo kitapatikana na hatia ya kukiuka kanuni za shirika la kimataifa la kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu.

Rais wa shirika la kimataifa la riadha – IAAF Sebastian Coe alionya kuwa huenda akaiondoa timu ya Kenya katika tamasha la Rio ikiwa hatua haitachukuliwa, baada ya Kenya kukosa kutimiza masharti hayo katika muda wa mwisho uliowekwa wa Februari 13

England Sebastian Coe
Rais wa IAAF Sebastian CoePicha: imago/ZUMA Press

Kaimu rais wa chama cha riadha Kenya Jackson Tuwei amesema nchi hiyo iko katika mkondo sahihi baada ya kuundwa shirikisho la kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu – ADAK, na ilipewa miezi miwili zaidi ya kuonyesha kuwa inafanya kazi yake. "tungependa kuona kuwa tunakamilisha ndani ya kipindi kilichowekwa, kwa sababu ni muhimu kuharakisha suala hilo. tungependa kumaliza suala hili haraka iwezekanavyo. bila shaka kwa kuzingatia haki binafsi za kila mtu. tungependa kuona kuwa mchezo wa riadha unalindwa kwa njia zote na kuwa nchi inakuwa safi, safi kutokana na mambo haya yote.

Tuwei ADAK inashughulikia mswada wa sera ambao utawasilishwa bungeni ili kuidhinishwa kuwa sheria.

Hali ya Kenya iliendelea kuwa mbaya mapema wiki hii wakati afisa mkuu mtendaji wa chama cha riadha Kenya alijiuzulu ili kuruhusu uchunguzi kufanyika kuhusiana na madai kuwa aliomba hongo kutoka kwa wanariadha wawili waliopigwa marufuku kwa muda, madai ambayo anayakanusha.

Tuwei anasema matokeo ya uchunguzi huo yanatarajiwa baada ya wiki mbili "tumekubaliana kuwa uchunguzi huu utafanywa na ADAK. kwa sababu ndilo shirika lililo na jukumu la kutoa elimu, uhamasisho na uchunguzi, na sasa vipimo, na ikiwa kuna chochote kinachostahili kufanywa, wana jukumu la kufanya hivyo. na kwa hivyo tumekubaliana sote kuwa ADAK itaunda kamati ya uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizi nilizotaja.

Mzozo wa matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu nchini Urusi na Kenya, pamoja na madai ya rushwa ndani ya shirika la IAAF, yameupaka tope mchezo huo kabla ya mashindano ya Olimpiki mjini Rio, Brazil ya mwezi Agosti.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP
Mhariri: Gakuba Daniel