1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kupambana na dawa za kuongeza nguvu

19 Desemba 2014

Bingwa mara tatu wa ulimwengu wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Moses Kiptanui ametoa wito wa kuchukuliwa adhabu kali kwa wanariadha wanaogundulika kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni

https://p.dw.com/p/1E7n3
40. Berlin-Marathon Wilson Kipsang Kiprotich 29.09.2013
Picha: picture-alliance/dpa

Kiptanui amesema tamaa ya “fedha nyingi” ndiyo chanzo cha udanganyifu huo unaoanza kuuchafua mchezo huo nchini Kenya. Wanariadha kadhaa wa Kenya wamethibitishwa kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita huku maafisa wa serikali wakisema idadi hiyo inayoongezeka ya visa vya matumizi ya dawa hizo inatokana na mawakala wa kigeni na shirikisho la riadha nchini Kenya Athletics Kenya – AK, kushindwa kuwahamasisha na kutoa elimu kikamilifu kwa wanariadha

AK imesema mapema wiki hii kuwa wanariadha wa masafa marefu wa Kenya Viola Chelangat Kimetto na Joyce Jemutai Kiplimo waligundulika kutumia dawa za kuimarisha nguvu mwilini, na watapigwa marufuku kwa miaka miwili, na ikaongeza kuwa vipimo vilivyofanyiwa wanariadha wengine watano vinatiliwa mashaka.

Kiptanui anasema visa vya matumizi ya dawa za kulevya vimepanda sana na akatoa wito kwa serikali kuweka sheria za kuwahukumia vifungo jela watakaopatikana na hatia.

Mwezi Oktoba, Mkenya Rita Jeptoo, mshindi wa mbio za marathon za Boston na Chicago, katika miaka miwili iliyopita, aligundulika kutumia dawa hizo. Mshindi wa mbio za marathon mwaka huu mjini London na New York Wilson Kipsang alikosa kufanyiwa vipimo vya dawa hizo mnamo mwezi Novemba 13 na akatakiwa na shirikisho la riadha ulimwenguni IAAF kutoa maelezo ya ni kwa nini. Hayo yalifichuliwa na shirikisho la riadha Kenya AK. Kipsang amelishutumu shirikisho hilo la AK kwa kukiuka maadili ya kitaaluma kwa kufichua suala hilo kwa umma.

Mwandishi. Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu