1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kupiga marufuku wasafiri kutoka Afrika magharibi

17 Agosti 2014

Kenya imekuwa moja kati ya nchi zilizochukua hatua ya kupiga marufuku wasafiri kutoka maeneo yaliyoathirika na ugonjwa wa Ebola katika Afrika magharibi na Nigeria yachukua hatua kuzuwia kusambaa kwa ugonjwa huo.

https://p.dw.com/p/1Cvuy
Kenya Airways Flughafen Nairobi ARCHIV
Shirika la ndege la Kenya litasitisha safari zake Afrika magharibiPicha: picture-alliance/dpa

Waziri wa afya wa Kenya James Macharia amesema jana Jumamosi(16.08.2014)kwamba nchi hiyo inafunga mipaka yake kwa wasafiri kutoka Guinea, Liberia na Sierra Leone, mataifa ambayo yameathirika zaidi na kuzuka kwa ugonjwa hatari wa Ebola.

Shirika la ndege la nchi hiyo Kenya Airways pia limesema litasitisha safari zake kwenda Freetown na Monrovia wakati hatua hiyo ya marufuku itakapoanza rasmi siku ya Jumatano.

Elfenbeinküste Felix Houphouet Boigny International airport Ebola Maßnahme
Hatua za kudhibiti Ebola katika uwanja wa ndege wa Felix Houphouet Boigny, Cote D'IvoirePicha: picture-alliance/dpa

Hatua hiyo imekuja huku wito ukitolewa kimataifa kusaidia kudhibiti virusi hivyo hatari, ambavyo tayari vimesababisha vifo vya watu 1,145 katika eneo la mataifa ya Afrika magharibi mwaka huu.

Nchini Uhispania, ambako mchungaji amefariki hivi karibuni kwa ugonjwa huo wa Ebola baada ya kuambukizwa nchini Liberia , mtu mwingine anafanyiwa uchunguzi kuhusiana na ugonjwa huo na amewekwa katika eneo la kutengwa katika hospitali jana Jumamosi.

Watu zaidi waambukizwa Nigeria

Waziri wa afya wa Nigeria Onyebuchi Chukwu amewaambia waandishi habari jana Jumamosi kuwa watu 12 wamepatikana na virusi vya ugonjwa huo hadi sasa, ikiwa ni pamoja na wanne ambao wameshafariki, wakati watu wengine 189 wanachunguzwa mjini Lagos na wengine sita katika mji wa kusini mashariki wa Enugu.

Ebola Krankenhaus Sierra Leone 11.08.2014
Katika hospitali nchini Sierra LeonePicha: picture alliance/AP Photo

"Kama mnavyofahamu, wagonjwa ambao wanatibiwa wamehamishiwa sasa katika wodi maalum yenye vitanda 40 iliyotengwa kwa ajili ya ugonjwa huo iliyotolewa na serikali ya jimbo la Lagos," amesema.

Waziri huyo ameongeza kwamba wagonjwa watano karibu wamepata nafuu lakini akaongeza kuwa dawa ya majaribio, nano silver , ambayo inalengwa kutumika kwa wagonjwa haijaidhinishwa na kamati ya taifa ya maadili inayohusika na utafiti wa afya.

Wafanyakazi wa kujitolea

Pia amesema Mnigeria wa kwanza kugundulika na virusi vya Ebola , daktari mwanamke, amerejea nyumbani baada ya kulazwa hospitalini.

Symbolbild - Ebola in Liberia
Maiti ikipelekwa kuzikwa LiberiaPicha: picture-alliance/dpa

Nigeria imetoa mafunzo kwa watu wa kujitolea 800 kusaidia kupambana na ugonjwa huo wa Ebola kufuatia wito uliotolewa na maafisa katika jiji la Lagos kupata watu wa kujitolea ili kuweza kudhibiti upungufu wa wafanyakazi wa hospitali kwa sababu ya mgomo wa wiki sita wa madaktari kuhusiana na mishahara.

"Watu wamekubali wito wetu wa msaada," amesema Hakeem Bello, msemaji wa gavana wa jiji la Lagos Babatunde Fashola.

"tumewapa mafunzo watu 800 wa kujitolea katika maeneo ya kufuatilia watu walioambukizwa, kutoa uelewa wa ugonjwa huo pamoja na kutibu ugonjwa huo wa Ebola," ameongeza.

Ebola Spanien Rückkehr Patient Miguel Pajares 07.08.2014
Mchungaji aliyefariki kutoka Uhispania akirejeshwa nchini humoPicha: picture-alliance/dpa

Wataalamu wanasema Ebola inasambaa kwa kiwango kikubwa na kufikia hatua ya kushindwa kuudhibiti ugonjwa huo katika eneo hilo, wakati shirika la afya ulimwenguni WHO limetangaza ugonjwa huo kuwa ni dharura ya kiafya ya kimataifa na imetoa wito wa msaada wa dunia.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Daniel Gakuba