1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Maelfu wajitokeza kujisajili kupata 'Huduma Namba'

Shisia Wasilwa, Dw, Nairobi17 Mei 2019

Maelfu wamejitokeza kupiga foleni kujiandikisha katika maeneo mbalimbali ya Kenya kupata nambari maalum, Huduma Namba.

https://p.dw.com/p/3IfAs
Registrierung Kenia Nairobi
Picha: DW/S. Wasilwa

Siku moja kabla ya kufungwa kwa zoezi la kusajili wakenya kupata nambari ya Huduma, maelfu wamejitokeza kupiga foleni kujiandikisha katika maeneo mbali mbali ya Kenya. Serikali nchini humo inashikilia kuwa haitaongeza siku ili Wakenya wote wapate kujiandikisha licha ya rai za Wakenya. Hata hivyo siku inapokaribia kukamilika ya kujisajili Wakenya wengi hawajui ni kwanini wanajiandikisha.

Kadhia ya kujitokeza dakika za lala salama kujiandikisha katika baadhi ya vituo…Foleni ndefu zilianza kushuhudiwa katika vituo mbali mbali vya kujisajili kwa nambari ya Huduma jijini Nairobi, kuanzia saa tisa za alfajiri.

Baadhi ya Wakenya wasema hawajui umuhimu wa Huduma Namba

Usajili wa Wakenya kupata nambari maalum maarufu kama Huduma Namba
Usajili wa Wakenya kupata nambari maalum maarufu kama Huduma NambaPicha: DW/S. Wasilwa

Zoezi hili linalokamilika siku ya Jumamosi, limekuwa llikiendeshwa kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa. Daniel Koskei ambaye aliamka saa tisa za asubuhi kujisajili katika moja ya vituo hapa Nairobi, hana ufahamu wa zoezi hili:

"Sijui umuhimu wa hii kitu, kwa sababu, serikali inasema tujisajili lakini hatujui umuhimu wake, unashindwa kwa sababu tuna vitambulisho vingi na sisi wenyewe hatujasema tumechoka kuvibeba.”

Wakenya walio na umri wa miaka sita na kuendelea wanasajiliwa kwa kupigwa picha na alama za vidole vyao pamoja na wazazi wao kuchukuliwa. Baada ya miezi mitatu watu waliosajiliwa watapa nambari maalum kwenye kadi. Hata hivyo kuna wale wanaohisi kuwa serikali ingetumia njia nyingine kwa usajili maanake kila mkenya aliye na umrii wa miaka 18 ana kitambulisho.

Wakenya wamehamasishwa vya kutosha?

Watungaji sera wanaamini Wakenya hawajahamasishwa vya kutosha kuhusu Huduma Namba
Watungaji sera wanaamini Wakenya hawajahamasishwa vya kutosha kuhusu Huduma NambaPicha: DW/S. Wasilwa

Hata hivyo kwa watungaji sera, wanaamini kuwa Wakenya hawajahamasishwa vya kutosha kama anavyoeleza Wavinya Nzioka ambaye ni mtungaji sera: "Tungepanda kujua, je, hii data yote inayowekwa kwa huduma namba itatumiwa wapi? Tutaweza kupata huduma gani ambayo hatupati kwa paspoti na kitambulisho?"

Huduma namba itasaidia serikali kufahamu idadi ya wageni pamoja na wananchi wake. Kupitia takwimu hizo, serikali itajipanga kwa mgao wa raslimali katika majimbo mbali mbali. 

Serikali inatarajia kuwasajili Wakenya milioni 35 zoezi hili litakapokamilika siku ya Jumamosi. Mpango huu uliogharimu shilingi bilioni sita ulizinduliwa na rais Kenyatta katika jimbo la Machakos, mwezi mmoja uliopita huku akiwahusisha viongozi wa upinzani kama njia ya kuwahamasisha Wakenya.