1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya na Tanzania zaangukia pua

Bruce Amani
24 Juni 2019

Kocha wa Algeria Djamel Belmadi amesema kuwa timu yake haipaswi kumtegemea tu nahodha wake Riyad Mahrez iwapo ingetaka kufanya vyema katika Kombe la Mataifa ya Afrika - Afcon 2019

https://p.dw.com/p/3Kzcn
Afrika Cup Algerien vs Kenia
Picha: picture-alliance/NurPhoto/U. Pedersen

Algeria iliibwaga Kenya 2 – 0 jana usiku katika mechi yao ya ufunguzi ya Kundi C ambapo Marhez alifunga bao la pili.

Mahrez mwenye umri wa miaka 28, anashiriki katika Afcon kwa mara ya tatu akiwa na Algeria, ambao walifika robo fainali ya 2015 lakini wakafanya vibaya katika duru ya kwanza miaka miwili iliyopita licha ya kuwa mojawapo ya timu zilizopigiwa upatu.

Kocha wa Harambee Stars Sebestine Migne alisikitishwa na mwanzo mbaya wa timu yake, hali ambayo walishindwa kabisa kujiondoa

Niliwaambieni kabla ya mashindano haya…nilikuwa mkweli tu. haiwezekano kushinda kombe hili. Hakuna kitu muhimu zaidi kuliko uzoefu. Na kama unataka kushinda mechi hapa, unahitaji kucheza kwa dakika 90. Tulicheza tu katika kipindi cha pili. Labda tulikuwa chini ya shinikizo. Tunapaswa kujifunza, lakini katika siku nne zijazo, itakuwa hadithi nyingine.

Afrika-Cup 2019 | Algerien vs Kenia
Mahrez aliifungia Algeria bao la piliPicha: Reuters/A. Abdallah Dalsh

Mechi nyingine iliyoihusisha timu ya Afrika Mashariki, Senegal iliimarisha hadhi yake ya kuwa mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu kushinda kombe la mwaka huu baada ya ushindi wa 2 – 0 dhidi ya Tanzania. Senegal haikonekana kumkosa kabisa Mshambuliaji Sadio Mane, ambaye alitumikia adhabu ya kufungiwa mechi moja. Mabao ya Simba hao wa Teranga yalifungwa na Keita Balde na Krepin Diatta. Aliou Cisse ni kocha wa Senegal "ni wazi kwamba katika mashindano ya aina hii, uzoefu ni muhimu sana. Tulicheza dhidi ya timu yenye wachezaji wengi wanaojua kudhibiti mchezo. Nadhani katika mchezo wa kandanda, suala kuu ni kuudhibiti mchezo kwa faida yako. Na ndicho hasa Senegal ilikifanya leo. Baadhi ya vijana wetu walicheza kwa mara ya kwanza katika mashindano ya aina hii na walileta kiasi Fulani cha uwoga katika timu yetu.

Kipa wa Tanzania Aishi Manula aliisaidia sana Taifa Stars kutopokea mabao mengi na hata kocha wake Emmanuel Amunike alikiri kuwa mipango yao haikufua dafu na kwamba walikutana na mpinzani mwenye uzoefu mkubwa sana. "Mpango wetu ulikuwa John Bocco. Tulimuweka kushoto kwa sababu alicheza mara kadhaa katika nafasi hiyo na tukajaribu kuipa nguvu safu ya kati, tukifahamu kuwa Wasenegal, aina yao ya mchezo ni kutawala safu ya kati. Kwa bahati mbaya kwetu, hatukumudu kuitawala safu ya kati ya Wasenegal, maana walikuwa huru sana. Mwishowe tukamuondoa mmoja wa viungo na kumuweka Bocco katikati, na kumleta Thomas Ulimwengu au Simon Msuva kwenye wingi. Katika kandanda, bila shaka unaposhindwa, unaweza kusema mbinu zako hazikufanya kazi. Unaposhinda, unasema mbinu zako zilifaulu.

Afrika Cup Senegal Tansania
Tanzania walishindwa kutamba mbele ya SenegalPicha: Reuters/A. Abdallah Dalsh

Katika mechi ya kwanza jana, Morocco ilipata ushindi wa 1 – 0 dhidi ya Namibia kupitia bao la kujifunga.

Hii leo, Ivory Coast, mabingwa wa mwaka 2015, watakuwa wa kwanza kuingia uwanjani dhidi ya Afrika Kusini, katika mechi ya kundi D.

Katika Kundi E,

Angola v Tunisia zinakabana koo ambpo zimekutana tu mara mbili katika historia ya michuano hii, na mara ya mwisho ilikuwa ni miaka 11 iliyopita nchini Ghana, ilipotoka sare ya kutofunga, matokeo ambayo yaliwasaidia kufika katika hatua ya robo fainali.

Kocha wa Tunisia Alain Giresse amesema lengo ya timu yake ni kufika katika hatua ya robo fainali ya michuano hii, licha ya kufahamu upinzani mkali.

Mali v Mauritania - Mali inaanza mechi ya ufunguzi, baada ya maafisa wa soka nchini humo kutishiwa. Aidha, kocha wa Mohamed Magassouba alichelewa kukitaja kikosi cha wachezaji wake wa mwisho kuelekea katika michuano hii.

Mauritania wamefuzu katika michuano hii kwa mara ya kwanza, na kocha Corentin Martins, raia kutoka Ufaransa anasema wachezaji wapo nchini Misri kushindana na kushinda mechi kadhaa.