1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaendelea kusubiri

Admin.WagnerD8 Machi 2013

Tume ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC, imelaumiwa kwa mwendo wa kinyonga katika kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais, huku baadhi ya vyama vya kisiasa vikidai kuwa kuna hila za kuiba kura.

https://p.dw.com/p/17tIg
Masanduku ya kura
Masanduku ya kuraPicha: REUTERS

Tume hiyo kufikia sasa imejumlisha matokeo ya maeneobunge 185 kati ya maeneobunge 291. Lakini mwenyekiti wake Issack Hassan amekanusha kuwepo na njama za kuiba kura, na kuongeza kuwa tume yake haijasukumwa na mtu yeyote kuchelewesha matokeo na wala haiupendelei upande wowote.

“Ningetaka kuwahakikishia kwamba kwa niaba ya tume, mwenyekiti na wanachama wengine wa Tume hii makamishna na wafanyikazi wa tume hawaegemei upande wowote tumekula kiapo kuhakikisha tunadumisha sheria kwa kutoa huduma bila upendeleo,” alisema Issack wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi.

Uhuru Kenyatta ameendelea kuongoza matokeo ya awali.
Uhuru Kenyatta ameendelea kuongoza matokeo ya awali.Picha: Getty Images

Uhuru bado ashikilia uongozi

Wananchi wamelalamika kwamba muda waliosubiri matokeo hayo ni mrefu mno, lakini waangalizi wa uchaguzi huo wamewataka wananchi kutoishinikiza tume ili iweze kufanya kazi yake kwa ufasaha zaidi. Hadi kufikia saa 12 na nusu asubuhi, mgombea Uhuru Kenya wa Muungano wa Jubili alikuwa akiongoza kwa kuwa na kura 4,334,917 dhidi ya kura 3,895,962.Lakini kura hizo zilikuwa ni kutokan majimbo 196 kati ya majimbo 291.

Maafisa wa uchaguzi wana muda hadi siku ya Jumatatu kutangaza matokeo kamili. Licha ya kasi ndogo ya kuhesabu kura, waangalizi wa kimataifa wamesema upigaji kura na zoezi la kuhesabu vimeendeshwa kwa uwazi. Ushindi wa moja kati ya moja wa wagomebea utamuhitaji apate asilimia 50 na zaidi, vinginevyo kutakuwepo na duru ya pili.

Mtihani kwa Kenya

Uchaguzi huo unatizamwa kama mtihani kwa taifa hilo lemye uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki, ambalo sifa yake kama demokrasia tulivu ilitiwa doa na umuagaji damu uliyofuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2007. Uchaguzi huu utategemea kama kama matokeo ya mwisho yatakubaliwa na pande zote, na endapo pingamizi zozote zitamalizwa mahakamani au mitaani.

Raila Odinga aombea majaaliwa.
Raila Odinga aombea majaaliwa.Picha: RODGER BOSCH/AFP/Getty Images

Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza wake William Rutto wanakabiliwa na mshtaka katika Mahakama ya kimataifa ya uhali ICC huko The Hague kwa kuhusika kwa njia moja au nyingine katika ghasia zilizozuka punde tu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Habari kutoka Mahakama ya ICC zinasema kwamba mahakama hiyo imeahirisha tarehe ya kuanza kwa kesi ya Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Balozi Francis kutoka tarehe 11 mwezi Aprili hadi tarehe 9 mwezi Julai mwaka huu. Jopo la majaji watano wanaosikiza kesi hiyo walikubali ombi la wakili Francis Kirimi wa Muthaura na Uhuru Kenyatta kwamba kesi yao iahirishwe hadi tarehe 9 mwezi ujao. Wakati huo huo Serikali imewataka wafanyikaziwote wa umma kuripoti kazini leo Ijumaa na kusubiri matokeo ya kura hiyo wakiwa kazini.

Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi/rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga