1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yafikiria sera ya mwanamke 1 watoto 2

6 Novemba 2013

Utafiti uliofanywa nchini Kenya umeonesha taifa hilo litashindwa kufikia dira yake ya maendeleo ya mwaka 2030 kutokana na wingi wa watu na sasa linataka kuanzishwa sera ya mwanamke kutozaa zaidi ya watoto wawili.

https://p.dw.com/p/1ACu4
Mtoto wa Kiafrika.
Mtoto wa Kiafrika.Picha: AP

Ripoti ya utafiti huo iliyopewa jina la "Uchambuzi wa Hali ya Idadi ya Watu nchini Kenya" na kuchapishwa rasmi mwishoni mwa mwezi uliopita na Wizara ya Mipango ya nchi hiyo, inasema haja ya watoto ni kubwa sana nchini humo na kwamba lazima idhibitiwe.

Maeneo kame ya kaskazini mwa nchi hiyo, licha ya kuwa kwake na shida kubwa zaidi ya maisha, yametajwa na ripoti hiyo kuwa yanayoongoza kwa idadi kubwa ya vizazi.

Ingawa ripoti hiyo haisemi moja kwa moja, lakini inaelekea sana kupendekeza sera ya kila mwanamke kuzaa watoto wawili nchini Kenya kuwa jambo la lazima.

Kazi kubwa zaidi yahitajika

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema kwamba hata kama sera hiyo itaanzishwa, italazimika kutanguliwa na mfumo mzuri sana wa kuisaidia, zikiwemo njia za kuimarisha uzazi salama, afya ya kimama na watoto wanaozaliwa na pia kampeni itakayokwenda hadi vijijini.

Watoto wa Kibera, Nairobi.
Watoto wa Kibera, Nairobi.Picha: picture-alliance/dpa

Kubwa zaidi ni kuhakikisha kuwa wasichana wengi zaidi kadiri inavyoyumkinika wanapatiwa elimu angalau mpaka ya sekondari, kwani utafiti huo ulionesha kwamba wanawake wenye watoto kidogo zaidi ni wale ambao angalau wamefikia kiwango hicho cha elimu.

Wakosoaji wa pendekezo hili la kuanzishwa kwa sera ya watoto wawili kwa kila mwanamke, wanasema kwamba hakuna uwiano kati ya idadi ndogo ya watu na kufikiwa kwa Dira 2030 inayoielekeza Kenya kuwa taifa lenye uchumi wa kati.

Mwandishi: Mohammed Khelef/standardmedia.co.ke
Mhariri: Josephat Charo