1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yapiga marufuku maandamano Nairobi, Mombasa na Kisumu

Shisia Wasilwa12 Oktoba 2017

Serikali ya Kenya imepiga marufuku maandamano katikati ya miji ya Nairobi, Kisumu na Mombasa kwa sababu ya usalama wa wananchi na mali. Imeonya kuchukua hatua dhidi ya waandaaji wa maandamano

https://p.dw.com/p/2lji9
Fred Matiangi vorne links
Picha: Imago/Xinhua Afrika

Serikali nchini Kenya imepiga marufuku maandamano kati kati ya miji ya Nairobi, Kisumu na Mombasa kwa sababu ya usalama wa wananchi na mali. Akiongea na wanahabari, Waziri wa Usalama Fred Matiangi amesema kuwa afisa mkuu mtendaji wa Muungano Mkuu wa Upinzani – NASA, Norman Magaya, atachukuliwa hatua za kisheria kwa maandamano yaliyofanyika jana jijini huku mali ya watu ikiharibiwa wa wengine kadhaa kulazwa baada ya kujeruhiwa. Hatua hiyo ni pigo kwa Muungano wa NASA baada ya kutangaza kuwa watakuwa wakifanya maandamano kila siku kuanzia juma lijalo. Upande wa NASA umesema hautayumbishwa na amri hiyo ya serikali.

Matiangi amesema kuwa hatua hiyo inafuatia mazungumzo na kamati ya ushauri ya masuala ya usalama iliyotaja maandamano hayo kuwa hatari na kulinganisha na bomu linasubiri kulipuka. Kwenye maandamano yaliyofanywa hapo jana na viongozi wa Muungano wa NASA, watu kadhaa walijeruhiwa na magari ya watu kuharibiwa pamoja na maduka yao.

Wafanya biashara walalamika

Polisi walipua gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji Nairobi
Polisi walipua gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji NairobiPicha: Reuters/T. Mukoya

Aidha waziri huyo amesema kuwa kabla ya kikao cha leo alikutana na jamii ya wafanyabiashara waliomfahamisha kuhusu athari za maandamano hayo. Matiang'i amesema "Hatutaruhusu maandamano kati kati ya miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu. Inspekta mkuu wa polisi ameshauriwa vya kutosha."

Hata hivyo, waziri huyu alikuwa mwepesi wa kusema kuwa hatua hiyo hailengi kukandamiza haki za kikatiba za wananchi kwani maandamano yaliyofanyika hayakuwa ya amani. Kufuatia uharibifu wa hapo jana kwenye maandamano, waziri huyo amewataka Wakenya walioathiriwa kupiga ripoti kwenye kituo cha polisi cha Nairobi.

Afisa mkuu mtendaji wa Muungano wa NASA, Norman Magaya, amelaumiwa kwa kutozingatia sheria alipokuwa akiitisha maandamano hayo. Matiangi anaongeza kusema "Tutamshtaki bwana Magaya na tunasubiri ripoti ya uharibifu uliotekelezwa ili tupate thamani kamili ya mali iliyoharibiwa."

Waandamanaji wa NASA wakimbia polisi walipofyatua gesi ya kutoa machozi
Waandamanaji wa NASA wakimbia polisi walipofyatua gesi ya kutoa machoziPicha: Reuters/T. Mukoya

NASA yasema haitayumbishwa

Kwa upande wake, Muungano Mkuu wa NASA umesema hautayumbishwa kwenye azma yake ya kushinikiza marekebisho kufanyika kwenye Tume ya Kusimamia uchaguzi siku 13 kabla ya uchaguzi kufanyika. Kwenye kikao na wanahabari Muungano huo umesema kuwa utaendelea kuandaa maandamano juma lijalo. Kwenye njia ya Simu mwenyekiti wa chama cha ODM John Mbadi amesema kwamba wataendelea kushinikiza tume ya kusimamia uchaguzi kufanya marekebisho kwa maandamano.

Wakenya wa matabaka mbali mbali pia wameelezea hisia zao kuhusu hali ya siasa ilivyo nchini Kenya. Wakati huo huo, Raila Odinga na mgombea mwenza Kalonzo Musyoka wameondoka nchini kwa ziara ya ng'ambo. Odinga ameelekea Uingereza huku Kalonzo akielekea Marekani. Maelezo ya safari zao hayajatolewa kwa ukamilifu. Viongozi hao wameelezea nia yao ya kushiriki kwenye maandamano hayo. Kwenye maandamano ya jana, viongozi hao hawakushiriki.

 

Mwandishi: Shisia Wasilwa/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef