1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yapiga marufuku mifuko ya plastiki

Grace Kabogo
16 Machi 2017

Kenya imepiga marufuku utengenezaji na uingizaji wa mifuko yote ya plastiki inayotumiwa kwa shughuli za kibiashara za kufungia bidhaa au kwa matumizi ya nyumbani.

https://p.dw.com/p/2ZHT1
Fukushima kontaminierte Erde Boden
Picha: picture-alliance/dpa/F.Robichon

Kenya imeingia katika orodha ya nchi ya hivi karibuni kuchukua uamuzi huo barani Afrika. Waziri wa mazingira Judi Wakhungu ametoa amri hiyo ya marufuku iliyochapishwa katika notisi rasmi ya serikali na kutangazwa hapo jana kwa umma.

Hatua hiyo mpya itaanza kutekelezwa miezi sita kutoka tarehe iliyochapishwa rasmi kiserikali yaani 28 Februari. Nchi za Kiafrika ambazo pia zimechukua au kutangaza uamuzi kama huo ni pamoja na Cameroon, Guinea Bissau, Mali, Tanzania, Uganda, Ethiopia, Mauritania na Malawi miongoni mwa nyingine.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya mazingira, UNEP limesema kwamba mifuko ya plastiki kwa muda mrefu imekuwa ni tatizo kubwa linalosababisha uharibifu wa mazingira na chanzo cha matatizo ya kiafya pamoja na kuua ndege, samaki na wanyama wengine.

 

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP
Mhariri: Saumu Yusuf