1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yasubiri matokeo ya mwisho kwa wasiwasi

11 Agosti 2017

Tume ya uchaguzi ya Kenya ilikuwa inajiandaa kutangaza matokeo ya mwisho Ijumaa katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali. Upinzani umedai ushindi na kuzusha taharuki katika taifa hilo.

https://p.dw.com/p/2i3Sb
Kenia Nairobi nach der Wahl
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Muungano wa upinzani - National Super Alliance (NASA) - siku ya Alhamisi uliitaka tume ya uchaguzi imtangaze mgombea wake Raila Odinga kuwa rais mteule, ukidai kuwa na ushahidi wa udanganyifu mkubwa uliopelekea matokeo ya awali kumweka mbele rais wa sasa Uhuru Kenyatta.

Waangalizi wa kigeni wamesifu mchakato wa uchaguzi huo walioutaja kuwa amani na wa wazi, lakini hali ilibadilia haraka na kuwa ya wasiwasi wakati Odinga alipokataa matokeo saa chache tu baada ya kuanza zoezi la kuhesabu kura.

Odinga alianza kulalamika kwamba matokeo yanayowasilishwa kwa njia ya kieletroniki yalikuwa hayafuatani na fomu zinazohitajika. Baadae alitoa maelezo ya madai ya udukuzi uliolenga kuchakachua matokeo hayo.

NASA baadae ikatoa madai mengine kwamba tume ya uchaguzi IEBC ilikuwa inaficha matokeo yalioko kwenye mtambo wake, ambayo, ilisema yanamuonyesha Odinga kuwa ndiye mshindi.

"Tunamtaka mwenyekiti wa IEBC atangaze matokeo ya uchaguzi wa rais mara moja na amtangaze Raila Amolo Odinga... kama raisa mteule," alisema mmoja wa viongozi wa NASA, Musalia Mudavadi.

Miito ya amani yahanikiza

Madai hayo yalichochea wasiwasi ambao umewafanya Wakenya kwenda taratibu tangu siku ya uchaguzi Jumanne, ambapo biashara nyingi zimefungwa, watumishi wa umma wakisalia nyumbani na kitaa ikiwa mitupu kwa sehemu kubwa. Matokeo ya mwisho yalitarajiwa kutolewa Ijumaa mchana.

Maandamano yamefanyika katika baadhi ya maeneo
Maandamano yamefanyika katika baadhi ya maeneoPicha: Getty Images/AFP/L. Tato

"Jaribio lolote la kuishinikiza IEBC, kama inavyoshuhudiwa, ni kinyume na sheria na linaweza kuchochea machafuko katika hali ambayo tayari imetawaliwa na wahka. Tumesema hivyo kabla, na tunarudia, kwamba mgombea yeyote mwenye malalamiko afuate njia zilizowekwa kisheria kushughulikia malalamiko yake," liliandika gazeti la Daily Nation katika tahriri yake.

"Mchakato wa kukamlisha uhakiki wa matokeo rasmi bado unaendelea, na kwa hivyo hakuna matokeo ya uchaguzi ambayo yanaweza kutumiwa kufungua shauri."

Maandamano yameendelea kufanyika tu katika ngome za Odinga katika maeneo ya mabanda promoka mjini Nairobi -- ambako polisi waliwapiga risasi na kuwauwa waandamanaji wawili siku ya Jumatano -- na katika mji wa Magharibi wa Kisumu.

Lakini kumbukumbu bado zingali mbichi, juu ya mgogoro uliosababisha machafuko ya kikabila na kisiasa yaliodumu kwa miezi miwili mwaka 2007-8, ambamo watu zaidi ya 1,000 waliuawa na wengine 600,000 kukoseshwa makaazi.

'Hatutaki vurugu, lakini tunataka haki'

Wakati veterani wa upinzani Raila Odinga, mwenye umri wa miaka 72, pia alidai ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2013 uliibwa, alipeleka malalamiko yake mahakamani na akaishia kukubali kushindwa.

Raila Odinga adai yeye ameshinda kura ya urais
Raila Odinga adai yeye ameshinda kura ya uraisPicha: Reuters/B. Ratner

"Hatutaki kuona vurugu zozote nchini Kenya. Tunajua madhara ya kilichotokea mwaka 2008 na hatutaki kuona marudio ya hali hiyo," Odinga alikimabia kituo cha televisheni cha Marekani, CNN katika mahojiano. Lakini alirudia kauli yake kwamba "simdhibiti yeyote. Watu wanataka kuona haki ikitendeka."

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alijibu madai ya NASA, na kusema ushahidi wao ulikuwa umejaa kasoro za kimahesabu na yalitoka katika kituo cha data cha Microsoft, wakati mfumo wa tume ya uchaguzi unatumia Oracle. IEBC inasisitza kuwa mfumo wa uchaguzi wa kielektroniki -- unaotazma kama njia muhimu y akuepusha udanganyifu wa kura, haukudukuliwa.

Uingereza na Marekani ziliungana na waangalizi wengine wa kigeni kuwasihi viongozi wa chama hicho kuwa na subira na kujizuwia kuchoche wasiwasi kuelekea kutolewa matokeo ya mwisho. Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, anaeongoza timu ya waangalizi kutoka kituo cha Carter, alielezea imani yake kwa IEBC.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Mohammed Khelef