1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yatakiwa ikome kuwafukuza Wasomali

8 Desemba 2010

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na Amnesty International yameitaka Kenya isitishe mpango wa kuwarejesha wakimbizi wa Kisomali katika taifa lao linalokabiliwa na vita na iwajibike kuwalinda

https://p.dw.com/p/QT1Y
Wakimbizi wa wa Kisomali nje ya vibanda vyao vya nyasi katika mji wa mpakani wa Kenya, ManderaPicha: AP

Masharika ya kutetea haki za binaadamu Human Rights Watch na Amnesty International yamesema serikali ya Kenya inafaa isitishe mpango wa kuwarejesha wakimbizi wa Kisomali katika taifa lao linalokumbwa na vita na iwajibike waziwazi kuwalinda na kuwasaidia. Kulingana na mashirika hayo wakimbizi 300 wa Kisomali wamerejeshwa nchini mwao katika kipindi cha wiki mbili za mwisho wa mwezi Novemba, kinyume na sheria ya kimataifa.

Duru za kuaminika na walioshuhudia matukio hayo ya kuwarejesha makwao wakimbizi wa Kisomali tarehe 29 na 30 Novemba, waliiambia shirika la kutetea haki za binaadam, Human Rights Watch kwamba maafisa wa polisi katika mji wa mpakani wa Liboi waliwasafirisha wakimbizi 130 waliotaka hifadhi ya ukimbizi hadi nchini mwao.

Tarehe 15 Novemba, Kenya pia iliwarejesha wakimbizi 140 kutoka katika mji wa Liboi. Wakimbizi hao walikuwa gerezani mjini Mombasa kwa kuwa nchini Kenya bila kibali. Wakimbizi wengi wanaotaka hifadhi ya ukimbizi nchini Kenya hupita katika mji huo wa mpakani wa Liboi.

Gerry Simpson ambaye ni mtafiti wa ukimbizi katika shirika la Human Rights Watch, amesema Kenya inakiuka haki ya Wasomali kwa kuwarejesha katika taifa lao lenye vita na ni kitisho kwa maisha yao. Bw Simpson amesema Kenya inafaa kutoa taarifa rasmi kwa viongozi wa mikoa na mabaraza ya miji kwamba wakimbizi wa Kisomali hawafai kurejeshwa katika nchi yao inayozongwa na vita.

Wakimbizi 130 waliorejeshwa kwao kutoka katika mji wa Liboi mwishoni mwa mwezi Novemba, hawangeweza kupelekwa katika kambi ya wakimbizi ya Daadab ambayo ina wakimbizi laki tatu kwa sababu magari ya kuwasafirisha yalikosekana. Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi, UNHCR liliipa idara ya ya masuala ya wakimbizi ya Kenya Lori litakalosaidia kuwasafirisha wakimbzi wanaotafuta hifadhi kutoka katika mji wa Liboi haki katika kambi ya wakimbizi ya Daadab.

Sheria ya kimataifa na ile ya kanda ya Afrika, inapiga marufuku kuwarejesha wakimbizi makwao kwa lazima na pia kuwatesa wanaotaka hifadhi. Ingawa Kenya inaweza kutetea hatua yake kama mkakati wa kiusalama, haiwezi kufunga mpaka wake na Somalia na kuwazuia wakimbizi wanaotafuta hifadhi. Tofauti na hayo, sheria ya Kenya ina kipengee kinachosema kwamba mtu yeyote ambaye sio Mkenya, ana haki ya kutorejeshwa katika eneo ambalo ni kitisho kwa maisha na uhuru wake na kwamba mtu kama huyo atachukuliwa kama mkimbizi.

Bw Simpson amesema Kenya inakiuka sheria yake na ile ya kimataifa pamoja na mapendekezo ya shirika linalowashughulikia wakimbizi, UNHCR kwamba mtu yeyote asirejeshwe kusini na au kati kati ya Somalia.

Michelle Kagari, naibu mkurugenzi wa kanda ya Afrika katika shirika la kutetea haki la Amnesty International, amesema vita vinavyotokota nchini Somalia, haviruhusu wakimbizi warejeshwe nchini humo. Shirika hilo la Amnesty International linasema kwamba Kenya iliwarejesha kiasi ya wakimbizi 8,000 nchini Somalia. Kumekuwa majadiliano ya muda mrefu kati ya Kenya na shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi, UNHCR kutaka nafasi ya ardhi iongezwe katika kambi ya wakimbizi ya Daadab lakini hadi kufikia sasa hakuna makubaliano yoyote.

Vita vya Somalia vimesababisha raia milioni moja kutoroka makwao na kundi la Al-Shabaab limekuwa likizua vurugu likikabiliana na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika wanaopiga diroa mjini Mogadishu.

Mwandishi: Peter Moss /dpa/HRW

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed