1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yatangaza majina ya magaidi

6 Oktoba 2013

Serikali ya Kenya imetaja majina ya watu 4 waliofanya shambulizi la kigaidi kwenye jengo la kibiashara la Westgate mjini Nairobi, na kutoa picha za video zinazowaonyesha magaidi hao ndani ya jengo walilolishambulia.

https://p.dw.com/p/19uJm
Mtafaruku ndani ya jengo la Westgate siku ya mashambulizi
Mtafaruku ndani ya jengo la Westgate siku ya mashambuliziPicha: Reuters

Msemaji wa jeshi la nchi hiyo, Meja Emmanuel Chirchir amesema mmoja wa magaidi hao ni Abu Baara al-Sudani, raia wa Sudan aliyepewa mafunzo na mtandao wa al-Qaida.

Mwingine ni Omar Nabhan, raia wa Kenya mwenye asili ya kiarabu aliyezaliwa mjini Mombasa, na kuhamia nchini Somalia akiwa na miaka 16. Gaidi wa tatu aliyetajwa ni Khattab al-Kene, msomali kutoka mjini Mogadishu ambaye anaaminika kuwa na mahusiano na kundi la al-Shabaab. Gaidi wa nne alitambulishwa kwa jina moja la Umayr; majina yeke mengine na uraia wake havikujulikana mara moja.

Picha za video

Picha za video zilizonaswa na kamera za usalama katika jengo la Westgate ambazo zimerushwa na televisheni nchini Kenya zimewaonyesha wanaume 4 wenye bunduki wakibeba mikoba ambayo inaaminika ilikuwa imejaa risasi, wakitembea tembea ndani ya duka kubwa na karibu na chumba cha kuhifadhia bidhaa.

Watu hao walionekana kutembea bila wasi, huku wakishikilia bunguki na kuzungumza katika simu za mkononi. Gaidi aliyetambulishwa na meja Chirchir kama al-Sudani alionekana kufungwa bandeji mguuni, ingawa alikuwa hachechemei.

Kundi la kigaidi la al Shabaab limekiri kuhusika katika shambulizi la Westgate
Kundi la kigaidi la al Shabaab limekiri kuhusika katika shambulizi la WestgatePicha: picture-alliance/AP

''Nathibitisha kuwa hawa ndio magaidi. Wote waliuawa katika operesheni'', Meja Chirchir aliliambia shirika la habari la Reuters, akikariri matokeo ya uchunguzi uliofanywa na jeshi la Kenya pamoja na idara za upelelezi za nchi hiyo.

Katika picha moja gaidi huyo alionyeshwa akipiga akipekuwa sehemu ya kuhifadhia fedha katika duka la Nakumat, na nyingine ilimuonyesha akitabasabu.

Magaidi 9 mbaroni

Serikali ya Kenya imesema kuwa wapiganaji wapatao 15 walihusika katika shambulizi la Westgate, na kwamba 9 kati yao wamekamatwa, na 5 wameuawa. Hata hivyo, watu walionusurika katika shambulizi hilo wamesema kuwa baadhi ya magaidi walifanikiwa kutoroka.

Mkuu wa Polisi ya Kenya David Kimaiyo aliiambia Reuters kuwa uchunguzi unaendelea, na yapo matumaini kuwa baadhi ya watuhumiwa watafikishwa kizimbani hivi karibuni.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya: Serikali yake imepania kuwafikisha kizimbani magaidi
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya: Serikali yake imepania kuwafikisha kizimbani magaidiPicha: John Muchucha/AFP/Getty Images

Kundi la al Shabaab la nchini Somalia lenye mafungamano na mtandao wa al-Qaida lilikiri kuhusika na shambulio la Westgate, na jana Jumamosi lilisema kambi yao katika mji wa Barawe kusini mwa Somalia ilishambuliwa na vikosi vya nchi ya Magharibi. Baadaye Marekani ilithibitisha kuwa makomando wa jeshi lake waliishambulia al Shabaab.

Mkuu wa zamani wa tume ya Umoja wa Mataifa ya uangalizi nchini Somalia na Eritrea Matt Bryden amesema al-Kene na Umayr wanajulikana kuwa wanachama wa kundi la al-Hijra, ambalo ni tawi la al-Shabaab nchini Kenya. Bryden amesema al-Hijra ni zaidi ya tawi tu la al-Shabaab, kwa sababu ilikuwepo hata kabla ya kundi hilo la nchini Somalia, chini ya mtandao wa al-Qaida.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE

Mhariri: Amina Abubakar