1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta, Ali na Muthaura kurudi ICC Septemba 21

8 Aprili 2011

Leo ilikuwa siku ya pili ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC, kuwasomea watuhumiwa wengine watatu madai kwamba walihusika kupanga njama iliyosababisha ghasia baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 Kenya.

https://p.dw.com/p/RGQr

Washukiwa hao Uhuru Kenyatta, Francis Muthaura na Hussein Ali walifika mahakamani mwendo wa saa nane na nusu alasiri. Watatu hao wanadaiwa kuwa waliipanga njama iliyosababisha ghasia baada ya uchaguzi mkuu katika maeneo ya Naivasha na Nakuru. Jaji anayeongoza mchakato dhidi ya watuhumiwa wa ghasia hizo Ekaterina Trendafilova, aliwaonya washukiwa hao wasitoe kauli za uchochezi zitakazoleta vurugu kwani kauli hizo zinaweza kuifanya mahakama ya ICC kutoa waranti wa kukamatwa kwao.

Kenia Wahlen Unruhen Gewalt Feuer
Vurugu baada ya uchaguzi mkuu Kenya 2007Picha: AP

Jaji Trendafilova, Alhamisi aliwasomea madai dhidi yao mbunge wa Eldoret Kaskazini William Ruto aliyekuwa waziri wa viwanda, Henry Kosgei na mtangazaji wa kituo cha redio cha Kass Fm Joshua arap Sang. Baadaye mahakama hiyo ilitangaza kwamba watatu hao wataijua hatma yao Septemba mosi ikiwa watasimama kizimbani kujibu kesi dhidi yao au la.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya

Mhariri: Josephat Charo