1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta asema hana nia ya kung'ang'ania madaraka

Shisia Wasilwa
2 Oktoba 2020

Rais Uhuru Kenyatta amekanusha madai kuwa atawania kipindi cha tatu baada ya kukamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho kulingana na katiba ya Kenya.

https://p.dw.com/p/3jKHh
Kenia Symbolbild Wahlen und Social Media
Rais wa Kenya Uhuru KenyattaPicha: AFP/T. Karumba

Akizungumza na kituo cha televisheni cha France 24, Kenyatta alisema lengo la kubadilisha katiba, ni kuwaleta wakenya pamoja kwa sababu ya amani, kwenye uchaguzi mkuu ujao. Wakati huo huo, Makamu wa Rais William Ruto, ameingia katika makao makuu ya chamacha Jubilee katika mtindo ambao washirika wa rais Kenyatta wameutaja kuwa mapinduzi.

Rais Kenyatta ameyakanusha madai hayo katika mazungumzo na kituo cha televisheni cha France 24 mjini Paris Ufaransa, akisema nia yake sio kung'ang'ania madarakani, bali kufanikisha amani ya kitaifa. Uhuru amesema: "Afadhali nije kufurahia likizo, hapa Ufaransa kila majira ya joto. Nimejitolea kufanikisha Amani, uthabiti na utajiri kwa watu wa Jamhuri ya Kenya.”

Rais Kenyatta ambaye yuko Ufaransa kwa ziara rasmi, amekariri kuwa huu sio wakati wa kampeini nchini Kenya na kwamba ni kipindi cha utendajikazi.  Makamu wake William Ruto hata hivyo ameonekana akifanya kampeini, huku akizuru pembe mbali mbali za taifa akijipigia debe, kabla ya uchaguzi mkuu ujao, jambo linaloongeza pengo kati yake na Rais.

Na siku moja baada ya Rais Kenyatta kuondoka nchini, makamu wake aliayavamia makao makuu ya chama cha Jubilee, huku akiwa amendamana na wabunge 38 wanaomuunga mkono. Wafuasia wa rais Kenyatta wamekitaja kitendo hicho kuwa cha mapinduzi.

Mrengo wa Ruto wakanusha madai ya kufanya mapinduzi kwenye chama cha Jubilee

Kenia Uhuru Kenyatta  William Ruto
Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William RutoPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Ruto ambaye alikataa kuzungumza na wanahabari, ameamua kuhudumu kwenye afisi hiyo mara mbili kwa juma, kama sehemu ya kuwatimua watu wanaoonekana kumpiga vita. Hakuna kiongozi yeyote wa chama hicho, akiwemo Katibu Mkuu Raphael Tuju, aliyemkaribisha. Seneta Mithika Linturi, aliyeandamana na Ruto, amekanusha madai ya kufanya mapinduzi chamani humo.

Linturi amesema: "Tulikuwa na mkutano mdogo kuhusu chama chetu, sababu nimeona kuna habari watu wanasema tumefanya mapinduzi katika chama. Hakuna mapinduzi ambayo tumeyafanya.”

Juma lililopita Ruto alipinga hatua ya chama cha Jubilee kujiondoa kwenye kinyang'anyori cha ubunge eneo la Msambweni na badala yake kuunga mgombea wa chama ODM kwenye uchaguzi mdogo. Siku moja baadaye Ruto alimpigia debe mgombea huru kuwania kiti hicho kinyume na msimamo wa chama chake.

Kukiwa kunasalia chini ya miaka miwili kwa rais Uhuru Kenyatta kukamilisha muhula wake wa mwisho wa utawala, mchakato wa mabadiliko ya katiba, unawapa mahasimu wake wa siasa, tumbo joto. Moja ya mapendekezo ya ripoti ya Mpango wa Maridhiano, maarufu BBI, baada ya ndoa ya siasa kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ni kuundwa kwa afisi ya Waziri Mkuu mwenye mamlaka na rais ambaye atachaguliwa na bunge.

Baadhi ya washirika wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta wamenukuliwa wakisema kuwa, rais Kenyatta atasalia kuwa rais, pindi, mpango huo utakapoidhinishwa na bunge. Waasisi wa mpango huo, wanashikilia kuwa, nafasi zitakazobuniwa kwenye utawala zitasaidia kupunguza ghasia ambazo hushuhudiwa kila baada ya uchaguzi.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, DW, Nairobi