1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry akutana na Lavrov Moscow

15 Desemba 2015

Marekani na Urusi zinahitaji kutafuta msimamo wa pamoja kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria pamoja na kurudisha hali ya utulivu na uthabiti Mashariki mwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/1HNjp
John Kerry na Sergei Lavrov wakisalimiana kabla ya mkutano wao
John Kerry na Sergei Lavrov wakisalimiana kabla ya mkutano waoPicha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Katika mazungumzo yanayoendelea mjini Moscow Kerry ambaye atakutana na rais Vladmir Putin baadae amesema ulimwengu utapata manufaa ikiwa nchi zenye nguvu zitakubaliana katika kuishughulikia kwa msimamo wa pamoja migogoro mikubwa.

Kerry amesema pamoja na kufahamu nchi yake na Urusi zimekuwa zikitafautiana kilicho wazi ni kwamba nchi hizo mbili zimeweza kushirikiana katika masuala kadhaa na kwamba katika mazungumzo ya leo anaweka matumaini kuwa msimamo wa pamoja utapatikana katika kukabiliana na hali ya mambo nchini Syria kwa kuwa kundi la IS ni kitisho kwa pande zote.

''Hawa ni mgaidi hatari zaidi,wanashambulia utamaduni wetu,historia na hata mwenendo wa maisha yetu na kwa hivyo hakuna budi bali nchi zilizostaraabika kusimama pamoja na kupambana ili kuwashinda na kuwaangamiza''

Mazungumzo kati ya Kerry na viongozi wa Urusi yanatazamiwa kuwa magumu hasa kwa kuwa nchi hizo mbili ziko kwenye mkwaruzano kuhusu suala zima la mchakato wa mpito wa siasa za Syria ambao unanuiwa kumaliza vita vya nchi hiyo pamoja na suala la mwelekeo wa kijeshi wa kupambana na kundi la itikadi kali la dola la kiislamu IS. Matokeo ya mkutano wa leo yataamua ikiwa mkutano wa kimataifa wa juhudi za kidiplomasia juu ya mgogoro wa Syria utafanyika kama ulivyopangwa siku ya ijumaa katika Umoja wa Mataifa au la.Tayari kwa upande wa Urusi waziri wa mambo ya nje Lavrov ameshadokeza msimamo wa nchi yake kuelekea suala la mgogoro wa Syria.

John Kerry na Sergei Lavrov wakizungumza na wanahabari Septemba mjini Geneva kuhusu Syria
John Kerry na Sergei Lavrov wakizungumza na wanahabari Septemba mjini Geneva kuhusu SyriaPicha: Philippe Desmazes/AFP/Getty Images

''Bila shaka mwafaka juu ya Syria unahitaji kuwepo muendelezo wetu wa kulishughulikia suala hili pamoja na juhudi zetu katika mwamko wa kuzingatia makubaliano yaliofikiwa Vienna''

Lavrov amegusia pia kuhusu kuwepo masuala kadhaa ambayo hayajatatuliwa na Marekani juu ya Syria kuhusiana na kipindi cha mpito wa kisiasa suala ambalo kimsingi linahitaji kufanikasha hatua ya kuwakutanisha wajumbe wa serikali ya rais Assad pamoja na wapinzani kwa ajili ya kushiriki mazungumzo kufikia mapema mwezi Januari.Ama kuhusiana na suala la mgogoro wa Ukraine nchi hizo mbili zimegawika kuhusu utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa Februari ambayo lengo lake lilikuwa kumaliza uhasama kati ya serikali ya Kiev na waasi wanaiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine.

-
-Picha: Reuters

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi amesema Marekani inapaswa kutumia ushawishi ilionao nchini Ukraine kuumaliza mgogoro na waasi kwa kuishawishi serikali na waasi kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano yanayokabiliwa na hali tete kabla ya kufanyika mageuzi ya kisiasa mashariki mwa Ukraine. Pamoja na hilo aidha nchi hizo mbili Urusi na Marekani zimeonekana kukubaliana kwamba kundi la dola la kiislamu ni kitisho kwa kila mmoja na kwa kila nchi.Ingawa vile vile awali kabla ya Kerry kuwasili Moscow Lavrov alisema kwamba nchi yake inategemea kuiona Marekani ikitathmini upya sera zake zinazoonekana kuyagawa mafungu makundi ya magaidi kwa kuyaona mengine kuwa mazuri na mengine mabaya.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Daniel Gakuba.