1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry awasili China, kituo chake cha pili

13 Aprili 2013

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, amewasili leo nchini China, katika juhudi za kuishawishi nchi hiyo kuishinikiza Korea Kaskazini kusitisha mpango wake wa nyuklia.

https://p.dw.com/p/18FET
Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry na Korea Kusini, Yun Byung-Se
Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry na Korea Kusini, Yun Byung-SePicha: Reuters

Kerry amewasili China ambayo ni kituo chake cha pili katika ziara yake ya Asia Mashariki, akitokea Korea Kusini, na anatarajiwa kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, kabla ya kukutana na Rais Xi Jinping, Waziri Mkuu, Li Kuqiang na viongozi wengine wa China.

Akiwa Korea Kusini jana Ijumaa (12.04.2013), Kerry alifanya mazungumzo na Rais Park Geun-Hye na kuahidi msaada wa Marekani katika mipango yake ya kuanzisha nia ya kufanya mazungumzo na majirani zake ili kutuliza hali ya wasiwasi inayoongezeka. Katika mkutano wake na maafisa wa chama tawala uliofanyika jana, Rais Park amesema Korea Kusini inapaswa kukutana na Korea Kaskazini, ilikuisikiliza nchi hiyo.

Kerry aahidi kumuunga mkono Rais Park

Wakati Kerry akiionya Korea Kaskazini kuachana na mpango wa kufanya jaribio la kombora, na kwamba nchi hiyo haiwezi kukubalika kama taifa lenye nguvu ya nyuklia, na kwamba kwa kufanya hivyo nchi hiyo itakuwa imefanya kosa kubwa, kiongozi huyo wa Marekani amesisitiza nia ya Marekani kuziunga mkono jitihada za Rais Park.

Rais wa Korea Kusini, Park Geun-Hye
Rais wa Korea Kusini, Park Geun-HyePicha: Getty Images

Kerry amesema Rais Park alichaguliwa kwa misingi tofauti ukiwemo uwezekano wa kuleta amani na kwamba Marekani inaheshimu hali hiyo. Amesema wamejiandaa kufanya kazi kwa imani kwamba uhusiano kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini utaimarika haraka.

Katika ishara nyingine ya kuonyesha kuwa Marekani ina matumaini ya kumaliza mvutano uliopo, Kerry hakutembelea kijiji cha makubaliano ya kusitisha mapigano cha Panmunjom, kituo ambacho kwa kawaida viongozi wa kigeni hukitembelea, pindi wanapozuru Seoul.

Marekani na Korea Kusini zatoa taarifa ya pamoja

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa kabla ya Kerry kuondoka Korea Kusini kwenda China, Marekani imesema imelipokea kwa mikono miwili pendekezo la mchakato wa kujenga uaminifu, lililowasilishwa na Rais Park. Hata hivyo, Kerry amesisitiza kuwa hatua ya kupunguza mvutano uliopo itahitaji ushirikiano kutoka pande zote na hasa China, ambayo kibiashara na katika masuala ya misaada imekuwa mshirika wa Korea Kaskazini tangu kumalizika kwa Vita Baridi.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita bila kuitaja nchi yoyote, Rais Xi alisema hakuna mtu atakayeruhusiwa kuiingiza nchi nyingine au hata dunia nzima katika machafuko kwa maslahi binafsi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, alisema jana kuwa viongozi wa China wana wasiwasi kutokana na mzozo katika rasi ya Korea na kwamba wanafanya kazi kuhakikisha wanapunguza mvutano uliopo.

Rais wa China, Xi Jinping
Rais wa China, Xi JinpingPicha: imago/Xinhua

Kerry anatarajiwa kuondoka China kesho Jumapili, kuelekea Japan, nchi ambayo inahusika kwa kiasi kikubwa na mzozo wa Korea Kaskazini na ambayo imeweka mitambo ya kuzuia makombora kuzunguka Tokyo, katika hatua za tahadhari, baada ya taarifa za kijasusi za Marekani na Korea Kusini kueleza kuwa Korea Kaskazini inajiandaa kufanya jaribio ya kombora lenye uwezo wa kuruka masafa ya kati.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri: Ssessanga Iddi Ismail