1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry kukutana na Putin mjini Sochi

Admin.WagnerD12 Mei 2015

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry atakutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin leo (12.05.2015) mjini Sochi. Uhusiano kati ya Urusi na nchi za magharibi umeanza kuimarika baada ya mvutano kuhusu Ukraine.

https://p.dw.com/p/1FOYC
Russland Sotschi US Außenminister John Kerry
Picha: Reuters/J. Roberts

Kerry anatarajiwa kuweka shada la maua katika kumbukumbu ya vita vikuu ya pili vya dunia katika mji wa mapumziko wa Sochi kabla kukutana na waziri wa mashauri ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov na rais Putin katika ziara yake fupi.

Ziara hiyo ya Kerry ndiyo ya kwanza kwa mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani tangu mzozo wa Ukraine kuibuka mwezi Aprili mwaka jana na kusababisha uhusiano kati ya Marekani na Ukraine kushuka kwa kiwango cha chini kabisa tangu enzi za vita baridi.

Putin amekanusha kuuchochea mzozo wa Ukraine ambao anatuhumiwa kuyatuma majeshi yake na vifaa vya kijeshi kuwasaidia waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo la mashariki ya Ukraine lakini amekubali yuko tayari kuboresha uhusiano na Marekani na Umoja wa Ulaya huku taifa hilo likihisi makali ya vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa kutokana na mzozo huo.

Russland Militärparade in Moskau
Picha: Reuters/Host Photo Agency/RIA Novosti

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema Kerry atakutana na Putin na baadaye atakutana pia na waziri mwenzake Sergei Lavrov. Msemaji wa wizara hiyo ya mambo ya nje wa Marekani Marie Harf amesema ziara hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kudumisha mawasilano ya moja kwa moja na maafisa wa ngazi ya juu wa Urusi na kuhakikisha mtazamo na maoni ya Marekani yamewasilishwa vyema.

Mizozo ya Ukraine, Syria na Iran katika ajenda

Miongoni mwa masuala yanayotarajiwa kujadiliwa kati ya Kerry na Putin ni mizozo ya Ukraine, Syria na Iran. Msemaji wa Putin hata hivyo amekataa kuthibitisha iwapo Putin atakutana na Kerry lakini wizara ya mambo ya nje ya Urusi imethibitisha Kerry atafanya mkutano na Lavrov.

Wizara hiyo imesema inatarajia ziara ya Kerry nchini Urusi itasaidia kurejesha mahusiano ya kawaida na Marekani ambao uthabiti wa dunia unautegemea kwa kiwango kikubwa. Naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Ryabkov amesema Kerry na Lavrov watajadiliana kuhusu utekelezaji wa mkataba wa kusitisha mapigano mashariki ya Ukraine ulioafikiwa Februari mwaka huu, pamoja na mizozo inayoendelea Mashariki ya Kati.

John Kerry und Sergei Lavrow in Genf Schweiz
Lavrov alipokutana na Kerry Geneva 02.03.2015Picha: Reuters/Evan Vucci/Pool

Viongozi hao hata hivyo hawatarajiwi kujadili vikwazo iliyowekewa Urusi na Marekani. Wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi imesema licha ya vikwazo vya mataifa ya Magharibi, makampuni ya Marekani bado yanataka kufanya biashara nchini Urusi.

Shirika la habari la Urusi Interfax limenukuu chanzo cha habari nchini humo kikisema kurekebisha mahusiano kati ya Urusi na Marekani itachukua miongo kadhaa. Chanzo hicho kimesema Marekani inatarajiwa kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kuutanzua mzozo wa Ukraine. Pia Urusi itaihimiza Marekani kuachana na kuipelekea silaha kali, ikilieza suala hilo kama la msingi.

Mwandishi:Caro Robi/DPA/AFP

Mhariri:Iddi Sessanga