1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi katika mauaji ya Khashoggi yaanza

Sekione Kitojo
3 Januari 2019

Waendesha mashitaka wa  Saudia watataka hukumu ya kifo dhidi ya watuhumiwa watano kati ya 11 walioko kizuwizini kuhusiana na  mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi, shirika la habari la Saudia SPA  limeripoti.

https://p.dw.com/p/3B0C3
Türkei Istanbul Protest gegen Ermordung von Khashoggi durch Saudis
Picha: Getty Images/AFP/Y. Akgul

Mahakama  ya  kifalme imesema  hayo wakati  ikifanya  kikao  chake  cha  kwanza  kusikiliza  kesi  hiyo.

Saudi Arabia  imesema  pia  imetuma  barua  kwa mwendesha mashitaka  wa  serikali  ya  Uturuki ikiomba "ushahidi  wowote unaohusiana  na  kesi  hiyo", ambayo  imeutikisa  uongozi  wa kifalme  nchini  Saudi  Arabia  na  kuchafua  heba  ya  mwanamfalme mteule Mohamed bin Salman  mwenye  umri  wa  miaka  33.

Saudi Arabien König Salman bildet Kabinett um | Kronprinz Mohammed bin Salman und König Salman
Mfalme wa saudia Salman akiwa pamoja na mwanamfalme Mohammed bin SalmanPicha: picture-alliance/AP Photo

Khashoggi alikuwa  karibu  na duru za jumba la ufalme  wa  Saudia kabla  ya  kuwa  mkosoaji  mkubwa  wa  mwanamfalme Mohammed na  kuanza  kuandika  katika  jarida  la  Washington Post na kuzungumza  katika  vyombo  vya  habari  vya  kimataifa  juu  ya siasa za  Saudia  na  hatimaye  kuhamia  nchini  Marekani mwaka jana.

Maafisa  wa  Saudia  wamekataa  shutuma  kwamba  mwanamfalme mteule aliamuru  kuuwawa  katika  ubalozi  mdogo  wa  Saudia  mjini Istanbul, ambamo  mwili  wa  Khashoggi  ulikatwakatwa, kuondolewa kutoka  katika  jengo  hilo  na  kukabidhiwa  kwa " mtu aliyeshirikishwa  nchini  humo" ambaye  hajajulikana.

Yaliko  mabaki  ya mwili  wa  Khashoggi  bado  hakujulikani, lakini televisheni  moja  ya  Uturuki  siku  ya  Jumatatu  ilionesha  watu wakibeba  masanduku  ambayo  huenda  yalikuwa  na  mabaki  ya mwili  wa  Khashoggi   na  kuingiza   katika  makaazi  ya  balozi mdogo  wa  Saudia  mjini Istanbul.

Saudi Arabien Kronprinz Mohammed bin Salman
Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa saudi ArabiaPicha: picture-alliance/AP Photo/G20 Press Office

"Kesi  hiyo  inayowahusu  watu  11 inayoanza  kusikilizwa  kwa mara  ya  kwanza  na  mwendesha  mashitaka  wa  serikali  katika kesi  ya  mauaji  ya  raia  Jamal Khashoggi  ilifanyika  leo, katika mahakama  ya  uhalifu  ya  kifalme  mjini  Riyadh," taarifa   kutoka katika  ofisi  ya  mwendesha  mashitaka  wa  Saudia  iliyochapishwa na  shirika  la  habari  la  SPA  ilisema.

Ofisi  ya  mwendesha  mashitaka  imesema  inataka  hukumu  ya kifo kwa  watu watano  kati  ya  11 walioshitakiwa.

Watuhumiwa  wengine  10  bado  wako chini  ya  uchunguzi. Shirika la  habari  la SPA  limeongeza  kwamba  wakili  wa  washitakiwa amehudhuria  kikao  hicho  na  mahakama  iliidhinisha  ombi la  watu hao  11  ambao  wameomba  kupatiwa  muda  zaidi  kuweza kutayarisha  utetezi  wao. Shirika  hilo  la  habari  hata  hivyo halikutoa  maelezo  zaidi  kuhusiana  na  kikao  kijacho.

Türkei l Fall Khashoggi l Türkische Polizei durchsucht Luxusvilla
Polisi wa Uturuki wakifanya upekuzi katika jengo la moja katika kijiji cha Samanli wakitafuta mabaki ya mwili wa Jamal KhashoggiPicha: Getty Images/AFP/Demiroren News Agency

Taarifa  hiyo  imesema  kuwa  nchi  hiyo  ya  kifalme inasubiri  jibu  la maombi juu  ya  taarifa  iliyotumwa  kwa  maafisa  wa  Uturuki.

Mwaka  uliopita, Mfalme  wa  Saudia Salman  alimteua  Ibrahim al-Assaf , waziri  wa  zamani  wa  fedha , katika  wadhifa  wa  waziri wa  mambo  ya  kigeni, katika  juhudi  za  kuimarisha  taswira  ya ufalme  huo  baada  ya  mzozo  huo uliosababishwa  na  mauaji hayo.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Grace Patricia Kabogo