1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KESI YA MAHARAMIA

Abdu Said Mtullya22 Novemba 2010

Kesi inayowakabili maharamia wa kisomali imeanza leo mjini Hamburg.

https://p.dw.com/p/QFVG
Maharamia 10 wa kisomali waliofikishwa mahakamani leo.Picha: dapd

Kesi ya maharamia kumi wa kisomali imeanza katika mji wa Hamburg kaskazini mwa Ujerumani.

Maharamia hao wanakabiliwa na madai ya kuiteka nyara meli ya makontena ya Ujerumani kwenye pembe ya Afrika.Hiyo ni kesi ya kwanza kuwakabili maharamia kwenye mahakama ya mji wa Hamburg baada ya miaka mia nne iliyopita.

Watu hao wamefikishwa mbele ya mahakama kujibu mashtaka ya kuiteka nyara meli ya makontena ya Ujerumani mapema mwaka huu kwenye bahari ya Hindi katika pembe ya Afrika.Watu hao waliokuwa wameshamiri kwa silaha waliingia ndani ya meli ya Ujerumani ,Taipan na kuiteka kwa muda wa saa nne kabla ya wanajeshi wa Uholanzi kuwakamata maharamia hao .

Mwendesha mashtaka Mkuu wa mji wa Hamburg Wilhelm Möllers amesema pana ushahidi wa nguvu dhidi ya wasomali hao kumi.

Mabaharia wa meli ya Ujerumani waliweza kutoka salama siku hiyo walipovamiwa kutokana na kujificha mnamo chumba cha dharura na kuizima injini ya meli. Kwa muda wa saa nne, meli yao ilikiwamo mnamo mikono ya maharamia ya kukombolewa na wanajeshi wa Uholanzi.

Mashtaka yanayowakabili maharamia hao10 ni pamoja na jaribio la unyang'anyi, na shambulio lililotishia usafirishaji wa baharini Ikiwa watapatikana na hatia wasomali hao watapewa adhabu ya juu kabisa, ya vifungo jela, kuanzia miaka 10 hadi 15. Adhabu iliyokuwa inatolewa katika mji wa Hamburg miaka 400 iliyopita kwa mtu aliepatikana na hatia ya uharamia, ilikuwa ya kifo ,kwa kukatwa kichwa.

Kwa muda wa miaka kadhaa pwani ya Somalia imekuwa inakabiliwa na baa la uharamia.Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la kimataifa linaloshughulikia usafirishaji wa baharini, meli 23 na mabaharia 500 kwa sasa wanashikiliwa na maharamia wa kisomali.

Kesi iliyoanza leo mjini Hamburg dhidi ya wasomali hao ilifanyika mbele ya mahakama ya watoto kwa sababu washtakiwa kadhaa wanadai kwamba walikuwa chini ya umri wa miaka 18 walipokamatwa mapema mwaka huu. Mawakili wa washtakiwa wamewatetea wateja wao kwa kusema kwamba uhalifu walioutenda umesababishwa na vurumai ya kisiasa nchini mwao- Somalia.

Mwandishi/Mtullya Abdu/AFPE/ZPR/

Mhariri/Othman Miraj/