1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Mursi yaahirishwa hadi Februari 1

8 Januari 2014

Kesi ya kuchochea mauaji inayomkabili rais wa zamani wa Misri aliyeondolewa madarakani na jeshi, Mohammed Mursi, imeahirishwa hadi Februari Mosi. Kesi hiyo imeahirishwa kutokana na hali mbaya ya hewa.

https://p.dw.com/p/1AmsY
Rais wa zamani wa Misri, Mohammed Mursi
Rais wa zamani wa Misri, Mohammed MursiPicha: picture alliance/AP Photo

Mwanzoni televisheni ya taifa ya Misri ilikuwa imeripoti kuwa Mursi alitarajiwa kufikishwa leo katika mahakama ya chuo cha polisi mjini Cairo kwa helikopta ya jeshi, ambako kesi yake ilitarajiwa kuanza kusikilizwa, lakini alishindwa kusafirishwa hadi mahakamani hapo.

Afisa mwandamizi wa polisi wa mji wa Alexandria, Nasr al-Abd, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa helikopta iliyokuwa imchukue Mursi, ilishindwa kuondoka katika gereza hilo kutokana na hali mbaya ya hewa.

Kikao cha leo kilipaswa kuwa cha pili

Kikao cha leo kilikuwa kiwe cha pili cha kesi inayomkabili Mursi ya kuchochea mauaji ya wanaharakati wa upinzani katika ghasia zilizotokea nje ya Ikulu mwaka 2012, wakati akiwa rais. Katika kikao cha kwanza hapo Novemba 4, mwaka jana, kesi ilishindwa kuendeshwa kwa sababu ya Mursi kukaidi amri za majaji.

Polisi wa kutuliza ghasia wakiwa mjini Cairo
Polisi wa kutuliza ghasia wakiwa mjini CairoPicha: Reuters

Katika kikao hicho, Mursi alisisitiza kuwa yeye bado ni rais halali wa Misri. Mursi anashtakiwa na wenzake wengine 14, wakiwemo wasaidizi wake wa zamani na viongozi wa chama chake cha Udugu wa Kiislamu.

Mahakama ya chuo cha polisi nje kidogo ya mji mkuu, Cairo, ndiyo ile ile inayosikiliza kesi ya mtangulizi wake, Hosni Mubarak anayetuhumiwa pia kwa makosa kama hayo.

Muungano wa vyama vyenye itikadi kali za Kiislamu, unaoongozwa na chama cha Udugu wa Kiislamu, ulikuwa umetoa wito kwa mamilioni ya wafuasi wake kuandamana wakati wa kesi hiyo. Kesi dhidi ya Mursi inaonekana kama mtihani kwa viongozi wapya wa Misri, ambao wamekuwa wakikosolewa kwa ukandamizaji.

Mauaji ya maelfu ya watu

Zaidi ya watu 1,000 wameuawa tangu Mursi aondolewe madarakani na maelfu ya wafuasi wake wamekamatwa. Imeelezwa kuwa uwezekano wa kupatikana kwa suluhisho la kisiasa katika taifa hilo la Kiarabu, uko mbali sana kufikiwa. Mursi pia ameshtakiwa kwa kuhusika na ujasusi na kusaidiana na wapiganaji kufanya mashambulizi nchini Misri.

Wafuasi wa Mursi wakiandamana mjini Cairo
Wafuasi wa Mursi wakiandamana mjini CairoPicha: picture alliance/AA

Mursi alichaguliwa kidemokrasia Juni mwaka 2012, baada ya Mubarak kuondolewa madarakani kutokana na vuguvugu la mapinduzi la mwaka 2011. Hata hivyo, mwaka wake mmoja madarakani uligubikwa na mizozo ya kisiasa, mapigano makali na kuyumba kwa uchumi.

Wakati huo huo, kiongozi wa kidini mwenye mafungamano na chama cha Udugu wa Kiislamu, Yusef al-Qaradawi, ametoa amri inayowazuia Wamisri kupiga kura ya maoni iliyoitishwa na serikali ya mpito iliyowekwa madarakani na jeshi, itakayofanyika wiki ijayo. Wafuasi wa Mursi wameshatoa wito wa kususiwa kwa kura hiyo iliyopangwa kufanyika tarehe 14 na 15 ya mwezi huu wa Januari.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef