1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya NPD dhidi ya rais wa Ujerumani

Christina Ruta25 Februari 2014

Kesi yenye utata wa kisiasa: Je, rais Joachim Gauck aliionyesha NPD kama vichaa? Mahakama kuu ya katiba ya Ujerumani inasikiliza kesi ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia dhidi ya rais wa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1BEnS
Chama cha NPD kimefulia mashtaka rais wa shirikisho la Ujerumani Joachim Gauck.
Chama cha NPD kimefulia mashtaka rais wa shirikisho la Ujerumani Joachim Gauck.Picha: picture-alliance/dpa

Mahakama kuu ya katiba nchini Ujerumani iliyoko mjini Karlsruhe, Jumanne hii (25.02.2014) inaanza kusikiliza kesi iliyofunguliwa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia NDP dhidi ya rais wa shirikisho Joachim Gauck. Chama hicho kinadai kuwa katika moja ya hotuba zake, rais Gauck alikiuka wajibu wake wa kutoegemea upande wowote wa kisiasa, kwa kuwafananisha wafuasi wa chama hicho na vifaa wanaopasa kupuuzwa.

Kesi hiyo inahusu hotuba aliyoitoa Gauck wiki chache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, kufuatia maandamano katika eneo la Hellersdorfer, ambalo wakaazi wake walikuwa wakipinga kuachwa nje katika siasa. Makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia yalitumia fursa ya maandamano hayo kuchochea chuki dhidi ya wageni, na hali hii iliyaweka maisha ya wakimbizi hatarini, ambapo polisi ililaazimika kuwakisindikiza wakati wakitoka na kurudi katika makaazi yao, tena kwa kupitia milango ya nyuma.

Rais Joachim Gauck, anaeshtakiwa na chama cha NPD.
Rais Joachim Gauck, anaeshtakiwa na chama cha NPD.Picha: picture-alliance/dpa

Siku chache baada ya kisa hiki, rais Gauck alitoa hotuba mbele ya wanafunzi wapatao 400 mjini Berlin, ambapo alichukuwa msimamo dhidi ya waandamanaji wenye itikadi kali katika kijiji cha Hellersdorf. Rais Gauck alisema wanahitaji raia wanaokwenda mitaani na kuwaonyesha wasokotaji mipaka yao.

Je, rais alikiuka wajibu wake wa kutoegemea upande?

Lakini swali ni je, kauli hiyo rais Gauck aliwalenga NPD kama wasokotaji? Volker Boehme-Nessler, profesa wa masomo ya sheria ya umma katika chuo kikuu cha sayansi cha mjini Berlin, anasema jambo la kuangalia ni iwapo rais Gauck alishawahi kulitumia neno wasokotaji kwa NPD. Inawezekana kuwa Gauck aliwaita waandamanaji wasokotaji lakini siyo NPD kama chama.

"Katika hali hii rais hakuilenga moja kwa moja NPD na kuishusha hadhi, lakini waandamanaji kwa ujumla. Katika hili mahakama inaweza kusema rais hajakiuka wajibu wake wa kutoegemea upande kwa sababu kauli yake haikuilenga NPD na wala hajaishushia hadhi.

Katika matamshi kama hayo, kinachoangaliwa ni muktadha, anasisitiza profesa wa sheria kutoka Berlin, Ulrich Battis, na kuongeza kuwa matamshi ya Gauck yanaangukia katika mpaka, na suala la iwapo mpaka huu umevukwa au la litaamuliwa na mahakama kuu ya katiba mjini Karlsruhe.

Karipio la mahakama linaweza kudhofisha nafasi yake

Kinachofanyika hii leo ni kuanza kusikilizwa kwa kesi ya msingi, na hukumu inatarajiwa katika kipindi cha miezi mitatu. Hakuna anaejua moja kwa moja matokeo ya kesi yatakuwaje, lakini Profesa Nessler anahisi kuwa majaji watasisitiza katika hukumu yao kuwa rais wa Shirikisho ana wajibu wa kuhakikisha kuwa haegemei upande wowote.

Majaji wa mahakama kuu ya shirikisho ya katiba mjini Karlsruhe.
Majaji wa mahakama kuu ya shirikisho ya katiba mjini Karlsruhe.Picha: AP

Ikiwa mahakama ya katiba ya shirikisho itatoa hukumu kwamba rais alikiuka wajibu wake wa kutoegemea upande, hii haitakuwa na madhara ya moja kwa moja kwa serikali kuu, na Boehme-Nessler anaamini rais hawezi kupoteza nafasi yake kwa sababu ya hukumu hiyo. Lakini anaongeza kuwa ukemeaji wa wazi unaweza kuwa tatizo kwa rais, kwa sababu hili linaweza kuidhoofisha nafasi yake.

Tofauti na raia wengine, rais wa shirikisho la Ujerumani hawezi kueleza maoni yake kwa uhuru zaidi, kwani anapaswa kuwa muunganishaji anaewaleta pamoja raia wote. Ofisi ya rais wa shirikisho la Ujerumani haina mamlaka kama ilivyo kwa rais wa Marekani au Ufanransa na badala yake, mamlaka yako kwa Kansela na bunge.

Rais anapaswa kuiwakilisha Ujerumani nje, na kuwaleta pamoja raia akiwa ndani ya nchi, hivyo hapaswi kuonekana anaegemea upande wowote, na hili ndilo litafsiriwa upya na mahakama kuu ya shirkisho ya katiba mjini Kahlsruhe.

Mwandishi: Anna Peters
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba