1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hata hivyo, Ntaganda amekana mashtaka yote dhidi yake

2 Septemba 2015

Kesi inayomkabili mbabe wa zamani wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Bosco Ntaganda inaanza kusikilizwa hii leo katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu-ICC.

https://p.dw.com/p/1GPyM
Bosco Ntaganda
Bosco NtagandaPicha: Reuters

Bosco Ntaganda, mwenye umri wa miaka 41, anakabiliwa na mashtaka 18 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu, ikiwemo ubakaji kwa wanajeshi watoto ndani ya jeshi lake mwenyewe.

Ntaganda, aliyekuwa kamanda wa waasi nchini Kongo, aliwasili leo kwenye mahakama ya ICC akiwa amevalia shati jeupe lenye mistari ya kijivu na alionekana mtulivu, huku akiwa ameketi kwenye kizimba akimsubiri Jaji Robert Fremr, aanze kumsomea mashtaka yake.

Ntaganda anatarajiwa kuzungumza na hivyo kuvunja ukimya kwa mara ya kwanza hadharani, tangu alivyojisalimisha bila ya kutarajiwa mnamo mwaka 2013.

Wakati wa kikao cha awali cha siku mbili, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, alitarajiwa kuwasilisha ufunguzi wa hoja upande wa mashtaka, na kisha upande wa utetezi utawasilisha kwenye mahakama.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bom Bensouda
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bom BensoudaPicha: CC BY-SA 3.0

''Upande wa mashtaka utawasilisha ushahidi kuonyesha kwamba tangu Aprili 2002, Bosco Ntaganda na wahusika wenzake, waliandaa mpango wa kulidhibiti eneo la Ituri kijeshi na kisiasa, kudhibiti maeneo ya raia na kuwaondoa raia kwenye maeneo hayo,'' alisema Bensouda.

Ntaganda ambaye ni mzaliwa wa Rwanda, ambaye amekana mashtaka yote dhidi yake, ya kuhusika na mauaji ya kinyama ya kikabila kwa raia, kaskazini-mashariki mwa jimbo la Kongo la Ituri mwaka 2002 hadi 2003.

Anahusika kwa kiasi kikubwa

Hata hivyo, waendesha mashtaka wamesema kuwa Ntaganda ambaye pia anahusika kwa kiasi kikubwa kwenye mzozo huo, ambao makundi ya kutetea haki za binaadamu yanakadiria kuwa yamesababisha vifo vya watu 60,000 tangu mwaka 1999.

Wakili wa Ntaganda, Stephane Bourgon, amesema mteja wake ataendelea kukana mshtaka dhidi yake, wakati wa kesi hiyo ambayo itatangazwa moja kwa moja kupitia redio za kijamii nchini Kongo. Bourgon leo amewaambia waandishi wa habari kuwa atawasilisha ushahidi wa kina. Wakili huyo amesema Ntaganda yuko katika hali nzuri na yuko tayari kutoa maelezo wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake.

Bensouda amesema Ntaganda aliwasajili mamia ya watoto kwenye jeshi lake na aliwatumia kwa kufanya mauaji na walikufa wakati wa mapigano. Ameongeza kusema kuwa wanajeshi wa kike walibakwa mara kwa mara. Waliokuwa wanajeshi watoto walitoa ushahidi huo.

Wanajeshi wa M23
Wanajeshi wa M23Picha: Simone Schlindwein

Waendesha mashtaka wamekusanya ushahidi wenye kurasa 800 na wanapanga kuwaita mashahidi 80, ambapo 13 kati yao wakiwa ni wataalamu na wengine ni waathirika. Mashahidi watatu watakaotoa ushahidi wao ni pamoja na watoto waliokuwa wanajeshi wakati Ntaganda akiwa kamanda wa kikosi cha waasi cha Patriotic Forces for the Liberation of Congo-FPLC.

Ntaganda ni mwanzilishi wa kundi la waasi la M23, ambalo lilisambaratishwa na serikali ya Kongo, mwishoni mwa mwaka 2013, baada ya uasi wa miezi 18 kwenye mkoa wa Kivu ya Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Ntaganda aliyekuwa mmoja wa watuhumiwa waliokuwa wakitafutwa sana kwenye eneo la kanda ya Maziwa Makuu, , alijisalimisha katika ubalozi wa Marekani kwenye mji mkuu wa Rwanda, kigali mwaka 2013 na kuomba kupelekwa The Hague.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef