1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Ratko Mladic yafunguliwa The Hague

16 Mei 2012

Kesi ya mauaji ya halaiki dhidi ya Mkuu wa majeshi wa zamani wa Waserbia wa Bosnia, Jenerali Ratko Mladic imeanza leo katika mahakama ya Uhalifu wa Kivita kwa Yugoslavia ya zamani mjini The Hague.

https://p.dw.com/p/14wGR
Former Bosnian Serb army commander Ratko Mladic attends his trial at the International Criminal Tribunal for the former Yugoslavia (ICTY) at The Hague May 16, 2012. Mladic, 70, appeared on Wednesday for his genocide trial looking confident, flashing a thumbs-up and clapping his hands as he entered the courtroom. REUTERS/Toussaint Kluiters/Pool (NETHERLANDS - Tags: POLITICS CRIME LAW)
Ratko Mladic Prozess Oberster Gerichtshof Den HaagPicha: REUTERS

Mladic anashitakiwa kwa kuongoza mauaji ya kikatili ya Waislamu 8,000 wengi wao vijana na watu wazima huko Srebrenica mnamo mwaka wa 1995. Hayo ndiyo mauaji ya kikatili zaidi tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia.

Ratco Mladic ambaye sasa ana umri wa miaka 70, ndiye mhusika wa mwisho katika vita vya eneo la Balkan katika miaka ya tisini kufunguliwa mashitaka katika mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa iliyokuwa Yugoslavia mjini The Hague.

Anatuhumiwa kwa kuchochea siyo tu wiki nzima ya mauaji ya kikatili mjini Srebrenica, bali pia kuzingirwa Sarajevo kwa miezi 43 ambapo zaidi ya watu 10,000 waliuwawa na walenga shabaha, na makombora.

Mashitaka 11
Orodha ya mashitaka 11 yanayomkabili Mladic kama Kamanda wa jeshi la Serbia katika vita vya Bosnia vya mwaka wa 1992 – 95 ni pamoja na mauaji ya halaiki, vitendo vya kigaidi, na uhalifu mwingine dhidi ya binadamu.

Mauaji ya maelfu yalifanyika mbele ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa waliotarajiwa kuweka ulinzi
Mauaji ya maelfu yalifanyika mbele ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa waliotarajiwa kuweka ulinziPicha: picture-alliance/dpa

Mladic alikamatwa mwezi Mei mwaka jana baada ya miaka 16 ya kuwa mafichoni, amekanusha mashitaka hayo akisema ni ya kuchusha mno akiongeza kuwa yeye ni mgonjwa sana hivyo hawezi kuendelea na kesi. Mahakama hiyo ilitoa tamko kwa niaba yake kwamba hana hatia.

Akiwa amevalia suti ya kijivu na tai nyeusi, Mladic aliwaamkua majaji na kuwashangilia wafuasi wake wakati akiingia mahakamani wakati kesi yake ikianza leo. Kila mara alionekana akiandika maelezo na hakuonyesha hisia zozote wakati waendesha mashitaka walianza kufafanua uhalifu anaodaiwa kufanya.

Jaji Kiongozi Alphons Orie wa Uholanzi alisema awali ya yote mahakama hiyo inatathmini kuhairisha kuwasilisha ushahidi, ambao untarajiwa kuanza tarehe 29 Mei, kutokana makosa kwa upande wa waendesha mashitaka katika kufichua ushahidi kwa upande wa mshtakiwa. Mwendesha mashitaka Demort Groome alisema hatapinga hatua yoyote ya kuhairisha ushahidi.

Uhalifu ulipangwa
Groome alifungua taarifa yake kwa kumwangazia mvulana mwenye umri wa miaka 14 ambaye babake na mjombake walikuwa miongoni mwa wanaume 150 waliouwawa na wanajeshi wa Waserbia wa Bosnia mwezi Novemba mwaka 1992. alisema mauaji yote yaliyofanywa mjini Srebrenica Mladic yalipangwa.

Mji wa Srebrenica, Bosnia Herzegovina ambako zaidi ya watu 8,000 waliuawa
Mji wa Srebrenica, Bosnia Herzegovina ambako zaidi ya watu 8,000 waliuawaPicha: picture-alliance/dpa/M. Schrader

Kisha akawaonyesha majaji mkanda wa video wa mauaji yaliyofanywa katika soko la Markale katika mji mkuu wa Bosnia, Sarajevo, ambapo watu kadhaa waliuwawa.

Alisema mashambulizi hayo yalikuwa mpango wa kuwaangamiza raia wasio wa Serbia katika ardhi ya Bosnia. Groome amesema waendesha mashitaka wataonyesha ushahidi kubainisha kuwa Mladic alichangia katika kila ya aina ya uhalifu huo. Jenerali huyo alikataa kutoa tamko mbele ya mahakama kuhusu mashitka hayo lakini anakanusha kufanya makosa yoyote, akisema kuwa alifanya hivyo kuwalinda Waserbia ndani ya Bosnia. Ikiwa atapatikana na hatia, Mladic anaweza kupewa kifungo cha juu cha maisha gerezani.

Kiongozi wa zamani wa kisiasa wa Waserbia wa Bosnia Radovan Karadzic tayari anaendelea na kesi yake katika mahakama hiyo.

Mwandishi: Bruce Amani/APE
Mhariri: Abdu Mtullya