1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya rushwa dhidi ya Jacob Zuma kusikilizwa leo.

4 Agosti 2008

Wafuasi wake wasema ni njama ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/Eq9U
Rais wa ANC na makamu wa rais wa zamani wa Afrika kusini Jacob Zuma.Picha: AP

Mahakama nchini Afrika kusini leo itaamua iwapo mashtaka ya rushwa dhidi ya Kiongozi wa chama tawala nchini Afrika kusini ANC Jacob Zuma yana uzito wowote.

Mamia ya wafuasi wa Bw Zuma, walijitokeza jana bila kujali hali mbaya ya hewa ya ubaridi na mvua kumuunga mkono mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 66, anayetarajiwa kuwa mrithi wa Rais Thabo Mbeki kama kiongozi wa taifa hilo .

Wafuasi wa Bw Zuma wamekula kiapo kuufunga kabisa mji wa Pietermaritzburg mashariki mwa mkoa wa Kwazulu-Natal mahala kunakofanyika kesi ya mwanasiasa huyo maarufu, ambaye ni mzaliwa wa mkoa huo.Lakini huenda kesi hiyo ikacheleweshwa, huku wanasheria wanaomtetea Bw Zuma wakitarajiwa kutaka ifutwe kabisa.

Zuma ambaye anaangaliwa na wengi miongoni mwa tabaka la watu masikini kuwa shujaa wao, aliingia mahakamani asubuhi ya leo akipitia mlango wa nyuma wa jengo la mahakama, akifaulu kuwapiga chenga wapiga picha waliokusanyika kwa wingi nje ya jengo hilo.

Hii ni mara ya pili ambapo dola imejaribu kumfungulia mashitaka Bw Zuma kwa makosa yanayohusiana na rushwa, baada ya jaji kutoa pigo kwa waendesha mashitaka katika jaribio lao lililopita 2006, alipoiita kesi hiyo dhidi ya mwanasiasa huyo maarufu kuwa janga.

Wafuasi wa Bw Zuma wanasema mashitaka dhidi yake ni ulipizaji kisasi kisiasa dhidi ya Zuma aliyemuangusha rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini katika kinyanganyiro cha kuwania Urais wa chama cha ANC Desemba mwaka jana.

Zuma alishtakiwa tena siku chache tu baada ya kuchaguliwa.Zuma anakabiliwa na mashitaka 16 kuanzia uvushaji fedha hadi shitaka kuu la kuhusika katika upokeaji hongo kwa kuliinda kampuni moja ya silaha ya Ufaransa Thint, katika uchunguzi juu ya mkataba wenye utata wa biashara ya silaha. Bw Zuma Anadaiwa kupokea rand 500.000 sawa na euro 68.000 kila mwaka kutoka kampuni hiyo .

Kiongozi huyo amesema awali kwamba kipatikana na hatia azajiuzulu. Zuma alifukuzwa na Rais Mbeki katika wadhifa wa Makamu wa rais wa Afrika kusini 2005 baada ya mshauri wake wa fedha wa zamani Schabir Shaik kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kutoa hongo.

Kwa upande mwengine kisa cha rushwa sasa kimemgeukia pia Rais Mbeki binafsi. Gazeti la Sunday Times toleo la jana liliripoti kuwa Bw Mbeki alilipwa rand milioni 30 kiasi ya dola milioni 4. 1 ili ahakikishe kampuni hiyo ya kijerumani ya ujenzi wa meli MAN Ferrostaal inapewa kandarasi moja kubwa.

Kwa mujibu wa gazeti hilo linalodai taarifa yake inatokana na uchunguzi wa miezi 6, Mbeki alimpa Zuma randi milioni 2 na nyengine kwa chama tawala cha ANC.