1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khalfan Ghailani atajwa kama 'muuaji wa halaiki'.

9 Novemba 2010

Ghailani anatuhumiwa kwa kupanga mashambulio ya kigaidi mjini Nairobi na Dar es Salaam 1998.

https://p.dw.com/p/Q2HC
Ghailani anakabiliwa na makosa 286.Picha: AP

Mshukiwa wa ugaidi, Ahmed Khalfan Ghailani ametajwa jana na mwendesha mashtaka katika mahakama ya Manhattan nchini Marekani kama 'muuaji wa halaiki'. Ghailani anatuhumiwa kuhusika katika miripuko ya mabomu mwaka wa 1998 katika balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania.

Katika mchango wake wa mwisho katika kesi hiyo, mwendesha mashtaka wa mahakama ya Manhattan, Harry Chertoff alisema Bw Ahmed Khalfan Ghailani ambaye alikuwa ameketi viti kadhaa upande wake wa kushoto, ni muuaji wa halaiki ambaye ana alama ya damu ya mamia ya watu mikononi mwake.

Ghailani, Mtanzania anayetokea Zanzibar, ana umri wa miaka 36 na anahusishwa pakubwa na kupanga miripuko ya mabomu katika balozi za Marekani mjini Nairobi na Dar es Salaam mwaka wa 1998 iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

Mshukiwa huyo alikana makosa hayo na anahusishwa pakubwa na mtandao wa Al-Qaeda katika kanda ya Afrika mashariki. Kesi yake ni ya kwanza ya washukiwa waliokuwa wameshikiliwa katika gereza la Guantanamo nchini Cuba, kusikilizwa katika mahakama ya kiraia.

Bild des ersten Guantanamo-Häftlings vor einem US Zivilgericht: Ahmed Ghailani
Ghailani, 36 amekanusha mashtaka dhidi yake.Picha: AP

Mahakama ya Manhattan ni hatua chache kutoka katika jengo la mnara wa World trade centre ambapo shambulio la kigaidi la Septemba 11 mwaka 2001, lilitekelezwa na wanachama wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda. Wachunguzi wanalinganisha uhusiano huo kama hatua kubwa ya kutanzua kitendawili cha mashambulizi ya kigaidi.

Rais Barack Obama wa Marekani alitoa amri ya kufungwa kwa mahakama ya kijeshi ya Guantanamo na washukiwa wanaoshikiliwa wafunguliwe mashtaka katika mahakama ya kiraia. Azimio hilo lilipingwa vikali na wachunguzi kadhaa wakidai kwamba uzito wa kesi hizo za ugaidi haufai kushughulikiwa katika mahakama za kiraia.

Jaji, Lewis Kaplan amesema kesi hiyo inaweza kuendelea hadi mwakani.

Khalfan Ghailani alikamatwa mwaka wa 2004 akiwa nchini Pakistan. Anakabiliwa na mashtaka 286 ya uhalifu yakiwemo mauaji na kupanga njama ya kutumia silaha za uharibifu mkubwa na akipatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Mshukiwa huyo alikuwa akihamishwa kutoka katika kambi moja hadi nyengine ya shirika la ujasusi la Marekani, CIA ambapo anasemekana aliteswa. Hatimaye aliondolewa kutoka katika gereza la Guantanamo nchini Cuba na kupelekwa mjini New York, Marekani mwaka jana. Kulingana na taarifa ya vyombo vya habari nchini Marekani, mwendesha mashtaka, Harry Chertoff aliliambia jopo la majaji wanaosikiza kesi hiyo, kwamba kuna ushahidi wa kutosha dhidi ya Khalfan Ghailani. Upande unaomtetea Ghailani haujawaita mashahidi dhidi ya wale wa upande wa mashtaka. Kesi hiyo itasikilizwa tena na jopo hilo wiki hii.

Bw Ghailani, akiwa na wenzake waliopanga mashambulio hayo ya mabomu, wanadaiwa walikimbilia Pakistan siku moja kabla ya miripuko kutokea.

Mashambulio hayo yalimtia kiongozi wa kundi la Al-Qaeda, Osama bin Laden katika darubini ya maafisa wa usalama wa Marekani. Osama na naibu wake, Ayman al-Zawahiri wako katika orodha ya washukiwa wakuu wanaosakwa kwa kupanga mashambulio ya kigaidi.

Mwandishi: Peter Moss/Reuters/dpa/AFP

Mhariri: Josephat Charo.