1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiasi watu 200 wakamatwa Kenya

1 Aprili 2014

Polisi nchini Kenya imewakamata watu kadhaa wanaotuhumiwa kuhusika na mashambulizi yanayodhaniwa kuwa ya kigaidi yaliyotokea mjini Nairobi jana Jumanne (31.03.2014).

https://p.dw.com/p/1BZVN
Jengo la mgahawa lililoripuliwa
Jengo la mgahawa lililoripuliwaPicha: picture-alliance/dpa

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya DW, Msemaji wa Polisi nchini Kenya, Zipporah Mboroki, amesema kuwa hadi sasa polisi imeshawakamata kiasi watu 200 wanaohusishwa na mashambulizi hayo yaliyotokea jana usiku kwenye eneo la Eastleigh linalokaliwa na idadi kubwa ya Wasomali, na kusababisha vifo vya watu sita na kuwajeruhi wengine 25, huku tisa kati yao wakiwa katika hali mbaya.

Miripuko hiyo imetokea ikiwa ni siku moja tu baada ya mtu anayedaiwa kuwa gaidi kuripukiwa na bomu alilokuwa akijaribu kulitengeneza katika eneo la Pangani, mjini Nairobi.

Bibi Mboroki amesema kuwa zoezi la kuwasaka washukiwa wa mashambulizi hayo, linaendelea kufanyika katika maeneo yote ya Nairobi na kwamba polisi imetoa wito kwa wananchi kuwapa habari kuhusu wahusika hao ili waweze kunaswa.

Miripuko ya jana usiku ililenga migahawa miwili na zahanati moja. Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Nairobi, Benson Kibue, amesema kuwa mipuko mmoja uliiporomosha kabisa ghorofa ya kwanza ya mgahawa huo na unaonekana kuwa ulitengenezwa na kitu ambacho ni kikubwa kuliko bomu la kutupwa kwa mkono.

Mwanamke aliyejeruhiwa na mashambulizi hayo akiwasili hospitali
Mwanamke aliyejeruhiwa na mashambulizi hayo akiwasili hospitaliPicha: Reuters

Idadi ya walioawa inaweza kuongezeka

Kamanda Kibue, amesema idadi ya waliouwawa katika mashambulizi hayo inaweza ikaongezeka kutokana na kifusi kikubwa katika eneo ulipo mgahawa huo. Miongoni mwa waliojeruhiwa ni wanawake.

Kwa mujibu wa polisi, wengi wa waliokufa walikuwa ndani ya mgahawa wakipata chakula cha jioni. Aidha, Bibi Mboroki amesema ili kuhakikisha hali ya usalama inaimarishwa nchini Kenya, jeshi la polisi linaendelea na doria na wanasaidiana na wananchi kuhusu kupata habari za wahalifu, kwani wanaishi miongoni mwao.

Eneo la Eastleigh ambalo lina wakaazi wengi wa asili ya Kisomali, umekuwa ukiandamwa na mashambulizi kadhaa ya mabomu ya kutupwa kwa mkono katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Hivi karibuni, polisi wa Kenya waligundua bomu kubwa ambalo lilikuwa ndani ya gari, katika mkoa wa Mombasa.

Kenya imekuwa ikishambuliwa na kundi la waasi la Al-Shabab lenye makao yake nchini Somalia tangu nchi hiyo ilipopeleka wanajeshi wake nchini Somalia kukabiliana na kundi hilo lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE,DPAE,The Standard Kenya
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman