1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kibaki yuko tayari kuzungumza na upinzani.

4 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CkQ7

Nairobi. Chama kikuu cha upinzani , nchini Kenya , cha Orange Democratic Movement ODM, kinatoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi mpya wa rais. Madai hayo yanakuja kutokana na matokea ya kuchaguliwa tena kwa rais Mwai Kibaki, ambayo yamezusha siku kadha za machafuko. Mgombea wa upinzani Raila Odinga pamoja na wafuasi wake wanadai kuwa kulikuwa na wizi wa kura katika uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita.Kibaki ametoa wito wa utulivu nchini na kutoa nafasi ya mazungumzo na wapinzani wa kisiasa baada ya ghasia za jana Alhamis.

Wakati huo huo rais Mwai Kibaki anasemekana kuwa yuko tayari kwa ajili ya kuundwa serikali ya muungano ili kumaliza mzozo huo wa uchaguzi lakini iwapo upinzani utatimiza masharti yake, amesema mshindi wa nishani ya amani ya Nobel Askofu Desmond Tutu wa Afrika kusini leo Ijumaa.

Tutu amesema kuwa kuna matumaini makubwa , wakati akijaribu kupatanisha mzozo ambao umesababisha watu 300 kuuwawa na kutishia kuharibu uchumi wa taifa hilo ambao ndio imara kabisa katika Afrika mashariki.

Licha ya mji mkuu Nairobi kurejea katika hali ya utulivu , magari yakionekana barabarani , polisi walifyatua mabomu tena ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji katika mji wa Bandari wa Mombasa kuwatawanya waandamanji wapatao 200 wanaopinga serikali leo baada ya swala ya Ijumaa.

Nayo Ufaransa imetoa tamko kali kuhusiana na uchaguzi huo, ikiunga mkono madai ya upinzani kuwa kulikuwa na wizi wa kura. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Bernard Kouchner amesema kuwa inaonekana kulikuwa na wizi wa kura kwa sababu , wengi wanaona hivyo , kama nchi za Marekani na Uingereza ambazo zina uzoefu mkubwa katika nchi hiyo.

Hali ya machafuko na mzozo wa kisiasa nchini Kenya pia umeathiri uchumi wa mataifa mengine ya Afrika mashariki na kati kwa kusababisha ukosefu mkubwa wa mafuta. Nchini Rwanda, jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na Burundi milolongo mirefu ya ununuzi wa mafuta imekuwapo katika vituo vya kuuzia mafuta kufuatia uamuzi wa serikali za nchi hizo kuamua kuweka mgao wa bidhaa hiyo.