1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kijana mwingine mweusi auwawa na polisi Marekani

27 Novemba 2014

Nchini Marekani video inayomuonyesha afisa wa polisi akimpiga risasi mtoto wa kiume wa miaka 12 mmarekani mweusi aliyekuwa amebeba bunduki ya bandia na kumuua imezusha ghadhabu nchini humo

https://p.dw.com/p/1Dv4b
Maandamano ya Feurguson 26.11
Maandamano ya Feurguson 26.11Picha: Reuters/E. Garcia

Video ya matukio yaliyoyonaswa katika camera za uchunguzi wa mitaani imeonyesha jinsi kijana Tamir Rice alivyopigwa risasi sekunde chache tu baada ya maafisa wawili wa polisi walipowasili katika mji wa Cleveland huko Ohio.

Ukanda wa sauti uliorushwa hewani katika vipindi vya televisheni kadhaa nchini Marekani unaonyesha kwamba awali ya tukio hilo kulikuweko mtu ambaye alianza kumchunguza kijana huyo wakati akichezea bunduki yake ya bandia na kuwaita polisi lakini akaripoti takriban mara mbili kwamba anadhani bunduki ile haikuwa ya kweli.

Lakini kwa upande mwingine sauti iliyotolewa ya mtu aliyekuwa akizungumza na polisi waliokuwa wakikimbia kuelekea kwenye eneo la kufanyika tukio hilo haikutaja kwamba shahidi huyu alihisi bunduki hiyo ni bandia.Ukanda huo wa Video umetolewa katika wakati ambapo ghasia zimepungua mjini Ferguson baada ya kushuhudiwa vurugu kubwa zilizochochewa na uamuzi wa jopo kuu la mahakama wa kutomtia hatiani polisi wa kizungu aliyehusika kumpiga risasi kijana mweusi aliyekuwa hana silaha.

-
Picha: Reuters/E. Nouvelage

Waandamanaji wachache walivumilia mvua na theluji nzito kuandamana hii leo nje ya idara ya polisi katika kitongoji cha St Loius ambako kijana Michael Brown aliuwawa Agosti 9. Ikumbukwe kwamba mauaji ya kijana huyo yaliyotokana na kupigwa risasi yalizusha wiki kadhaa za maadamano na ghadhabu pamoja na mijadala kuhusu uhusiano kati ya watu wa rangi tafauti nchini Marekani pamoja na mbinu za kijeshi zinazotumiwa na polisi.

Siku ya Jumatatu wiki hii jopo kuu la mahakama ya Missouri lilipitisha uamuzi wa kutomtia hatiani afisa wa polisi Darren Wilson aliyemfyetulia risasi kijana Brown na kumuua hatua iliyoibua hasira miongoni mwa wamarekani na hata maandamano na ghadhabu zilishuhudiwa London Uingereza.

Kufikia Jumatano usalama ulikuwa bado umeimarishwa lakini hali ya mambo imeonekana kutulia hii leo na kurudi ya kawaida. Hata nchini Uingereza maelfu ya watu waliokasirishwa na unyama uliofanywa dhidi ya kijana Michael Brown waliandamana mjini London pia wakibeba mabango yaliyoandikwa nyanua mikono juu hakuna kufyetua risasi. Aidha hii leo watetezi wa haki za binadamu nchini Marekani wameitisha maandamano zaidi siku ya Jumamosi . Maandamano kama hayo yalifanyika mwaka jana baada ya mashtaka ya mauaji dhidi ya mlinzi George Zimmerman kufutiliwa mbali licha ya kumuua kwa kumpiga risasi kijana mmarekani mweusi,Trayvon Martin aliyekuwa hana silaha huko Florida.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman.