1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikao cha 65 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

15 Septemba 2010

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limeanza kikao chake cha 65 chini ya uongozi wa rais mpya,Joseph Deiss.

https://p.dw.com/p/PCNL
Kikao cha awali cha Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: AP

Ujumbe wake kwa viongozi hao ni kuchukua jitihada zote kupambana na matatizo yanayoukabili ulimwengu yakiwemo maendeleo,masuala ya afya na juhudi za kupambana na umasikini,.Kikao hicho cha kilele kinawaleta pamoja viongozi wa kisiasa wa mataifa 192 wanachama wa Umoja wa Mataifa.Wakati huohuo Umoja wa Ulaya umeshindwa kulishawishi baraza hilo kuupa nafasi muhimu zaidi katika masuala ya kidiplomasia kwenye vikao vyake.

Katika ufunguzi rasmi wa Baraza hilo,Rais wake mpya Joseph Deiss aliuelezea umuhimu wa kuyatimiza malengo yake katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.Bwana Deiss aliyaelezea matumaini yake kuwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linaweza kutoa mchango mkubwa katika masuala ya ulimwengu.Alisema ijapokuwa,''Aghalabu maoni ya wengi ni kuwa Umoja wa Mataifa ni shirika lililo na Baraza kuu ambalo halina makali,ni mahala pa kuzungumza tu bila ya kupitisha maamuzi yanayoleta mabadiliko.''

UN Vollversammlung Pakistan NO FLASH
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akilihutubia Baraza Kuu mwezi wa AgostiPicha: AP

Miradi endelevu

Baada ya ufunguzi huo wa kikao cha 65,Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Joseph Deiss aliwasisitizia waandishi wa habari umuhimu wa kuiimarisha miradi ya maendeleo inayoambatana na hali halisi ya mazingira bila kusababisha madhara zaidi.Aliligusia pia suala la athari za mabadiliko ya hali ya hewa na umuhimu wa kuwa na juhudi za pamoja kwani,''Hakuna manufaa yoyote ya nchi moja kuchukua hatua za kipekee ilhali mengine yanaendelea kama awali bila ya kujali hali halisi,''alifafanua.

Maendeleo na Usalama

Masuala mengine muhimu aliyoyafafanua ni kufanya mabadiliko katika Umoja wa Mataifa,kuzitathmini hatua zilizopigwa za kuyatimiza malengo ya maendeleo ya Milenia na pia kuipa kipa umbele miradi endelevu inayoyalinda mazingira.Malengo hayo ya maendeleo yalizinduliwa rasmi mwaka 2000 na azma ni kuyatimiza ifikapo mwaka 2015.Baadhi ya malengo hayo manane ni kuupunguza umasikini ulimwenguni kwa nusu,vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga,kusambaa virusi vya HIV na maambukizi pamoja na elimu kwa watoto wote wa kike na kiume.

UN Vollversammlung NO FLASH
Viongozi wakiwa kwenye kikao cha 64 cha Baraza La Usalama la UNPicha: picture-alliance/dpa

Kikao maalum cha kuzitathmini hatua hizo kimepangwa kufanyika ifikapo tarehe 23-25 mwezi huu na kitawaleta pamoja marais na viongozi wa mataifa.Ajenda ya kudumisha amani na usalama kote ulimwenguni pia imepewa umuhimu katika kikao hicho.Uturuki iliyo mwenyekiti wa zamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa itaongoza kikao maalum kitakachojadili mbinu za kuuimarisha mchango wa wanachama katika kudumisha amani ulimwenguni. 

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-AFPE/DPAE

Mhariri: Sekione Kitojo.