1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikosi cha Obama kuanza kuzipitia idara mbali mbali

13 Novemba 2008

Ni kumuandalia ripoti pamoja na makamu Joe Biden kabla ya kushika madaraka mwezi Januari

https://p.dw.com/p/FttJ
Rais mteule Barack Obama na Makamu wake Joe Biden.Picha: AP/DW-Montage

Wanasiasa wa ngazi ya juu, mabalozi wa zamani ,wafanyabiashara mashuhuri pamoja na wanasheria,wataiongoza timu maalum ya Rais mteule wa Marekani Barack Obama kuzipitia taasisi na vyombo vya serikali, Kabla Obama hajashika rasmi hatamu za uongozi baada ya kuapishwa Januari 20 .

Taarifa zinasema wataalamu wa masuala ya kijeshi wakiwemo waliokua maafisa wa ngazi ya juu katika utawala wa rais wa zamani Bill Clinton wanapanga kuandaa mambo katika wizara ya fedha, mambo ya nchi za nje na ulinzi.

Hata Ikulu White House nayo itapitiwa na kuchunguzwa , huku kikundi hicho cha watu 450 kikiingia katika idara na taasisi zaidi ya 100. Taarifa ya kamati ya Bw Obama ilisema lengo ni hatimae kumpatia Rais huyo mteule na makamu wake Joe Biden taarifa zinazohitajika kwa ajili ya sera na mikakati, masuala ya bajeti (matumizi ya serikali) na maamuzi ikiwa ni kabla ya kuapishwa kwake.

Akikabiliwa na vita viwili,Iraq na Afghanistan pamoja na hali mbaya kabisa ya kiuchumi tangu msukosuko wa kiuchumi wa miaka ya 1930, Obama anataka kuwa na uwezo wa kutekeleza mageuzi haraka iwezekanvyo, mara tua baada ya kushika hatamu Januari 20. Obama ameeleza wazi kwamba hali mbaya ya uchumi ni suala atakalolipa kipa umbele .

Hadi sasa rais huyo mteule amemteuwa tu mnadhimu mkuu wa shughuli za Ikulu Rahm Emmanuel, lakini kumekuweko na fununu na uvumi unaozidi juu ya ni nani atakayekua waziri wa fedha, mambo ya nchi za nje na ulinzi.

Miongoni mwa wanaotajwa kama waziri wa fedha ni Josh Gotbaum, ambaye wakati huu ni mshauri wa fuko la uekezaji linaloshughulika na marekebisho.

Katika wizara ya mambo ya nchi za nje wanaotajwa ni pamoja na Seneta John Kerry, gavana wa New Mexico Bill Richardson na Mrepublican mstaafu Chuck Hagel na pia Waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje katika awamu ya kwanaza ya utawala wa Bush, Colin Powelle, ambao wote ni maveterani wa vita vya Vietnam.

Obama alipata uungaji mkono kutoka kwa mtu asiyetarajiwa, pale aliyekua mgombea mwenza wa Mrepublican John McCain, Bibi Sarah Palin alipokiambia kituo cha televisheni CNN Jumatano kwamba itakua ni heshima kwake kuwa tayari kumsaidia rais mpya Obama na utawala mpya kwa njia yoyote ile, ikiwa ataombwa kufanya hivyo.

Viongozi wa dunia wanajiandaa kuanza kuwasili Washington leo (Ijumaa) kwa mkutano wa kilele wa kundi la nchi 20 tajiri na dola kuu kiuchumi utakaoanza kesho (Jumamosi), ulioitishwa na Rais George.W.Bush kusaka njia za kuurekebisha mfumo wa fedha duniani. Lakini wale wenye hamu ya kukutana na rais mteule Obama watavunjika moyo, kwani hatohudhuria mazungumzo hayo, akiheshimu usemi wake kwamba kuna rais mmoja tu katika wakati husika na hivi sasa bado ni Rais Bush.

Badala yake lakini waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wakati wa utawala wa Clinton ,Bibi Madeleine Albright na mbunge kutoka chama cha Republican Jim Leach watamuakilisha Obama kukutana na viongozi wa kigeni, kandoni mwa mkutano huo wa kilele.

Mbali na matatizo ya kiuchumi yanayotokana na msukosuko wa fedha duniani,mada nyengine katika mkutano huo wa viongozi mjini washington ni pamoja na vita vya Irak na Afghanistan.