1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Hagupit chaleta madhara Ufilipino

Abdu Said Mtullya7 Desemba 2014

Kimbunga kikali kimeikumbuka Ufilipino na kuziharibu nyumba na kusababisha mawimbi makubwa katika sehemu yote ya mashariki mwa nchi. Watu wachache tu wamekufa kulinganisha na maafa ya mwaka uliopita.

https://p.dw.com/p/1E0TC
Kimbunga cha Hagupit kimeleta madhara makubwa
Picha: picture-alliance/AP Photo/F.R. Malasig

Kimbunga hicho kinachojulikana kama Hagupit kimesababisha madhila zaidi kwa mamilioni ya Wafilipino baada ya maafa mengine makubwa. Kimbunga Hagupit kilichokuwa na kasi kubwa iliyosababisha upepo uliofikia mwendo wa kilometa 210 kwa saa, kilianzia kwenye bahari ya Pasifik kwenye kisiwa cha Samar katika jimbo la kati.

Asasi ya mambo ya hali ya hewa, Pagasa imesema kuwa dhoruba hiyo ni kubwa kuliko nyingine zote zilizoikumbwa Ufilipino mnamo mwaka huu. Nguvu ya dhoruba hiyo ni kubwa kuliko kimbunga kilichotokea mnamo mwezi Julai kilichosababisha vifo vya watu zaidi ya 100 nchini humo.

Nyumba zafigiliwa mbali na mitandao ya nishati yavurugika

Maafisa wa serikali wamesema watu wacheche wamekufa na mamilioni wameachwa gizani kutokana na umeme kukatika. Meya wa mji wa Catbalogan ameliambia shirika la habari AFP kwamba nyumba nyingi na hasa katika sehemu za pwani zilifagiliwa mbali na pepo kali.

Umeme umekatika katika sehemu nyingini za Ufilipino kutokana na nguzo za umeme kuanguka
Umeme umekatika katika sehemu nyingini za Ufilipino kutokana na nguzo za umeme kuangukaPicha: picture-alliance/dpa

Meya huyo Stephanie Uy-Tan amearifu kwamba miti na milingoti ya umeme imetenguka juu chini. Amesema mapaa ya nyumba pia yameng'olewa na kwamba sasa pana mafuriko.

Serikali yachukua hatua haraka kuwahamisha watu

Kutokana na wasi wasi wa kutokea tena kimbunga kama kile cha Haiyan kilichosbababisha vifo vya watu zaidi ya 7350, mwaka uliopita,serikali ya Ufilipino safari hii ilipitisha juhudi kubwa ya kuwahamisha watu mapema ambapo mamilioni walipatiwa hifadhi.

Matumaini ya kuepuka maafa makubwa yalijitokeza baada ya nguvu ya kimbunga Hagupit leo kuanza kupungua sana hadi kufikia kasi ya kilometa 170 kwa saa. Dhoruba hiyo imetabiriwa kuchukua muda wa siku tatu ambapo itazikumba hasa sehemu masikini za majimbo ya kati na wahusika wanafanya matayarisho ya kukabiliana na hali mbaya kabisa.

Hapo awali serikali ilitahadharisha juu ya kushtadi kwa dhoruba hadi kufikia urefu wa mita tano katika sehemu fulani na kusababisha mafuriko, maporomoko ya ardhi na pepo kali zenye nguvu za kuzing'oa hata nyumba madhubuti.

Madarasa yafungwa kwa muda shuleni

Katika mji mkuu Manila wenye wakaazi milioni 12 serikali imeyafunga madarasa kwa wiki ijayo katika muktadha wa utabiri wa mvua mkubwa katika mji huo hapo Jumatatu. Mamilioni wengine wanaishi katika mkondo wa kimbunga, ikiwa pamoja na wale walipo katika sehemu za kati za Philipinnes.Watu hao bado wanajaribu kuyajenga upya maisha yao baada ya kukumbwa na maafa ya kimbunga Haiyan kichotokea miezi 13 iliyopita.

Mamia kwa maelfu wamezikimbia nyumba zao na kuwekwa kwenye hifadhi za dharura
Mamia kwa maelfu wamezikimbia nyumba zao na kuwekwa kwenye hifadhi za dharuraPicha: Reuters/R. Montes

Licha ya kuleta madhara kwa watu, kimbunga Hagupit kimesababisha watu 650,000 wayakimbia makaazi yao na kuenda kwenye hifadhi za dharura. Wanajeshi 12,000 walifanya matayarisho kabambe ya ili kuepusha kabisa madhara kwa watu.

Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine kadhaa zimeahidi kuisadia Ufilipino endapo yatatokea maafa. Kamishna wa Umoja wa Ulaya Christos Stylianides anaeshughulikia misaada ya kibinadamu amesema Umoja huo utawapeleka wataalamu wake nchini Ufilipino ili kutathmini kiwango cha madhara na msaada ambao Umoja wa Ulaya unaweza kuutoa. Kamishna Stylianides amesema Ufilipino haipo peke yake wakati huu ambapo inakabiliana na hali ngumu.

Mwandishi: Mtullya Abdu/afp/dpa

Mhariri: Elizabeth Shoo