1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kina mama wajitolea kuimarisha usalama mitaani Kenya

14 Januari 2019

Wanawake wanaoishi maeneo ya mabanda nchini Kenya wamejitolea kukabiliana na ukosefu wa usalama katika maeneo yao, jukumu ambalo kwa muda mrefu liliachiwa wanaume.

https://p.dw.com/p/3BWzh
Der Slum Kibera in Nairobi
Picha: CC/Schreibkraft

Wanawake wanaoishi maeneo ya mabanda nchini Kenya wamejitolea kukabiliana na ukosefu wa usalama katika maeneo yao, jukumu ambalo kwa muda mrefu liliachiwa wanaume. Kupitia mpango walioupa jina ‘wamama na usalama' wanawake hao wanasema wanatambua jukumu lao kubwa la kuielekeza jamii ndiposa wanataka kuwa mstari wa mbele katika harakati za kukabiliana na ukosefu wa usalama. 

Maeneo ya mabanda yanasifika kwa kila aina ya uhalifu hali inayochangiwa na wingi wa watu, umasikini na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira. Kina mama na watoto huathirika zaidi kutokana na visa vya uhalifu katika maeneo hayo huku vijana wakilaumiwa zaidi kwa kusababisha uhalifu. Khadija Ali, mama na mkaazi wa eneo la mabanda la Kaptembwa mjini Nakuru, anaelezea baadhi ya changamoto ambazo kama kina mama wamekuwa wakizishuhudia katika maeneo haya.

Azma ya kutaka kubadili hali yao imewafanya kina mama hawa kuungana na kutafuta mbinu ya kukabiliana uhalifu. Chini ya mpango walioupa jina ‘wamama na usalama' kina mama hawa wameweka mikakati ya kuangazia changamoto za kiusalama zinazowasibu. Josephine Maritim anakariri kwamba kwa kuwa kina mama ni kiungo muhimu katika kuielekeza jamii, maovu katika jamii yanaweza kushughulikiwa iwapo watahusishwa kikamilifu katika utungaji wa sera muhimu.

Baadhi ya wasichana katika mtaa wa Kibera Kenya wakipata mafunzo ya namna ya kujikinga na kujilinda wanapovamiwa.
Baadhi ya wasichana katika mtaa wa Kibera Kenya wakipata mafunzo ya namna ya kujikinga na kujilinda wanapovamiwa.Picha: DW/J. van Loon

Jane Josiah kutoka Shirika la Midrift Human Rights linalohusika na maswala ya haki ya usalama anasema ni muhimu kwa sauti ya wanawake kusikika hasa katika maswala ya usalama. Anasema mpango huu ni muhimu katika kuziba pengo lililoko na kuimarisha ushirikiano kati ya idara ya usalama nchini na kina mama katika jamii, hasa kwa kuwawezesha kuelewa changamoto zao.

"Ilionekana kuwa wanawake walikuwa wachache sana katika juhudi hizi kiasi kwamba sauti ya wanawake haikuwa inasikika na hata iliposikika, haikuwa inapewa uzito sawa na ile ya wanaume. Jamii imejitolea sana kushirikiana na kina mama hawa na inadhihirika wanawake hawa wanaposema wameshuhudia mabadiliko."

Uhalifu nchini Kenya unaripotiwa kuongezeka huku miji ya Nairobi, Nakuru, Mombasa na Kisumu ikiathiriwa zaidi. Takwimu za  jeshi la polisi nchini Kenya zinaonyesha kuwa visa vingi vya uhalifu viliripotiwa mwaka 2018 ikilinganishwa na mwaka 2017.

 

Mwandish: Wakio Mbogho, DW Nakuru

Mhariri: Iddi Ssessanga