1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinshasa, Kampala zaunga mkono mpango wa ndege zisizo na rubani Kongo mashariki

12 Januari 2013

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Uganda zimeunga mkono pendekezo la vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, la kupelekwa kwa ndege za uchunguzi zisizo na rubani katika mpaka wa mashariki mwa Kongo.

https://p.dw.com/p/17Imm
Ndege isiyotumia rubani. Vikosi vya amani nchini Kongo vinataka kupatiwa ndege hizi tatu ili kusimamia vizuri mpaka wa mashariki mwa Kongo.
Ndege isiyotumia rubani. Vikosi vya amani nchini Kongo vinataka kupatiwa ndege hizi tatu ili kusimamia vizuri mpaka wa mashariki mwa Kongo.Picha: dapd

Umoja wa Mataifa unasema uasi wa miezi tisa uliyoirudisha nchi hiyo yenye utajiri wa madini katika vita, unaungwa mkono na nchi za Rwanda na Uganda, madai ambayo yanakanushwa na serikali za nchi zote mbili.

Kiongozi wa kisiasa wa M23 Jean-Marie Runiga akihutubia wakaazi wa Bunagana mashariki mwa Kongo.
Kiongozi wa kisiasa wa M23 Jean-Marie Runiga akihutubia wakaazi wa Bunagana mashariki mwa Kongo.Picha: AP

Herve Ladsous, mkuu wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, alisema wiki iliyopita kuwa ameliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa ndege tatu zisizo na rubani kufanya doria katika mpaka wa eneo la mashariki lenye milima, baada ya maelfu ya wanajeshi wa kulinda amani kushindwa kuwazuia waasi kuuteka mji muhimu wa Goma Novemba mwaka uliyopita.

Kinshasa yaukaribisha, Uganda yatoa masharti, Rwanda yaukataa

Msemaji wa serikali ya Kongo Lambert Mende alisema serikali yake inakaribisha mpango huo. Mende ambaye pia ni waziri wa mawasiliano aliwaambia waandishi wa habari mjini Kinshasa kuwa matumizi ya ndege hizo yatavisaidia vikosi vya kimataifa kuboresha usimamizi wa mpaka wenye matatizo unaozitenganisha Kongo na Rwanda.

Kampala ambayo ni mwenyeji wa mazungumzo kati ya serikali ya Kongo na waasi licha ya madai kuwa inawafadhili waasi, iliunga pendekezo hilo kwa tahadhari kwa masharti kwamba ndege hizo hazitumiki katika mashambulizi. Waziri wa ulinzi wa Uganda Chrispus Kiyonga alisema kama ndege hizo zitatumika kwa uchunguzi na kuheshimu uhuru, hilo litakuwa sawa.

Kwa upande wake, Rwanda ambayo ina kiti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imesema inaupinga mpango huo hadi  pale utakapofanyiwa tathmini. Naibu balozi wa Rwanda katika  umoja huo alionya kuwa Afrika isigeuzwe kuwa maabara ya vifaa vya uchunguzi kutoka mataifa ya kigeni.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu kushiriki kwa Rwanda

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ilisema mwaka uliyopita kuwa Rwanda ilituma vifaa na wanajeshi kupitia milima inayozitenganisha nchi hizo mbili kwa lengo la kuwasaidia waasi wa M23, ambao ilisema wanapokea amri kutoka kwa maafisa wa ngazi za juu nchini Rwanda, akiwemo waziri wa ulinzi. Rwanda ilikanusha vikali ripoti hiyo na badala yake, ikaigeuzia kibao Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa kushindwa kuwamaliza waasi wa Rwanda waliyoko nchini humo.

Waasi wa M23 wakiondoka katika mji wa Goma Disemba 1, 2012.
Waasi wa M23 wakiondoka katika mji wa Goma Disemba 1, 2012.Picha: Phil Moore/AFP/Getty Images

Licha ya kumalizika rasmi kwa vita vya kanda vilivyohusisha mataifa kadhaa jirani, sehemu kubwa ya mashariki mwa Kongo iko chini ya udhibiti wa makundi ya waasi wenye silaha na wanamgambo wanaotuhumiwa kwa ubakaji na mauaji. Karibu miaka miwili ya ukosefu wa utulivu imeacha mamilioni ya raia wa Kongo wakiwa wameuawa.

M23 na tangazo la kusitisha mapigano

Kundi linalodhibitiwa na Watutsi la M23, ambalo lilipewa jina lake kutokana na makubaliano ya amani ya Machi 23, 2009, yaliyopelekea waasi wa zamani kuingizwa katika jeshi la Kongo, lilianzisha tena uasi kwa madai kuwa serikali imeshindwa kuheshimu makubaliano hayo. Baadaye lilipanua madai yake na kutishia kusonga mbele kuiangusha serikali ya Rais Joseph Kabila.

Viongozi wa M23 wametangaza katika hatua ya upande mmoja ya kusitisha mapigano siku ya Jumanne, kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya mazungumzo na serikali mjini Kampala, hatua ambayo imeongeza matumaini ya suluhu ya muafaka kukomesha uasi huo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre

Mhariri: Sekione Kitojo.