1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinyan'ganyiro cha mshindi 3

9 Julai 2010

Ujerumani yaumana kesho na Uruguay,Paul asemaje ?

https://p.dw.com/p/OEyu
Pweza "Paul" alipoagua ushindi wa Spian dhidi ya Ujerumani.Picha: AP

"Paul"-Pweza kutoka Oberhausen, Ujerumani, aliegonga vichwa vya habari duniani kwa kuagua sawa sawa : ni timu gani itashinda, anatazamiwa hivi punde kutoa utabiri wake ni timu gani itaibuka bingwa wa dunia hapo Jumapili kati ya Spain na Holland. Na tangu Holland hata Spain, wanasubiri kwa hamu "Paul" atasema nini leo.Mashabiki wa Ujerumani hawajali tena vipi Paul anaagua leo mpambano wa kesho wa kuania mshindi wa 3 kati yao na Uruguay utakavyomalizika huko Port Elizabeth. Hata hivyo, mpambano huo unaahidi msisimko mkubwa, kwani Wauruguay, mabingwa wa kwanza wa dunia , wanataka kuthibitisha kwamba hatua walizopiga katika kombe hili la dunia haikuwa bahati nasibu tu.

Ujerumani na Uruguay , zimeshapambana mara 3 katika kombe la dunia na matokeo ya hadi sasa, yameonesha Wauru wanapokutana na Wajerumani, kila mara wanazidi nguvu.

Mpambano wa mshindi watatu huko Port Elizabeth , unaoitwa "finali-ndogo" ya Kombe la dunia , alao kwa Uruguay, utakuwa ni kilele cha dimba lao baada ya Kombe la dunia lililowasangaza mashabiki wengi ulimwenguni kwa matokeo iliopata Uruguay huko Afrika kusini.

Endapo Uruguay, ikiishinda Ujerumani , mabingwa hawa marambili wa dunia (1930 na 1950), watakuwa wamefika mbali kabisa tangu kupita miaka 40. Kwani, 1954 na 1970 Uruguay, ilimalizia nusu-finali.

Ujerumani, haitataka chochote kasoro ya ushindi hapo kesho ili kukamilisha Kombe hili la dunia kwa ufanisi. Bila ya ushindi , Kombe la dunia mwaka 2010 licha ya kusifiwa mno na ushabiki mkubwa wa wapambe wake, litakuwa pigo kwa Ujerumani baada ya kumaliza makamo-bingwa 2002 huko Korea ya kusini na Japan na nafasi ya 3 nyumbani, Ujerumani mwaka 2006.

Changamoto ya kwanza kabisa kati ya Ujerumani na Uruguay, ilikuwa Julai 23, 1966 huko Shefield, Uingereza, pale timu hizi mbili zilipochuana katika robo-finali. Ujerumani ikashinda kwa mabao 4:0.

Timu hizi mbili zikakumbana tena katika Kombe la dunia, 1970 huko Mexico kuania mshindi watatu kama hapo kesho. Kinyume na changamoto ya 1966, mpambano huu ulimalizikia ushindi wa bao 1:0 wa Ujerumani.

Ujerumani na Uruguay, zikakutana tena kwa mara ya tatu katika Kombe la dunia huko huko Mexico,1986. Mara hii Uruguay, ilizima vishindo vya Ujerumani katika duru ya kwanza na kugawana pointi zilipoachana sare bao 1:1.

Bingwa wa dunia 1990, stadi wa Ujerumani, Andreas Brehme, amesema kuwa, mshangao mkubwa wa Kombe hili la dunia, 2010 , ni kufika mbali sana kwa Uruguay. Hakuna bingwa yoyote wa dimba huko Amerika kusini kwenye wazimu wa dimba, alieweza kubashiri hayo. Kwani katika kundi lao, timu zilizopigiwa upatu kutamba ni makamo-bingwa wa dunia-Ufaransa na Mexico. Hata wenyeji, Bafana Bafana, waliokuwa pia kundi hili, walitazamiwa kuwapiku Wauruguay.

Mwishoe, Uruguay iliparamia kileleni mwa kundi lake katika duru ya kwanza na shukurani kwa mkono wa Suarez, katika lango lao walipocheza na Ghana, Uruguay, imefika umbali wa kucheza mpambano wa mshindi watatu na Ujerumani kesho.

Iliosalia sasa ni kusubiri kuona hivi punde, nini "Paul", pweza wa Oberhausen, ameagua juu ya hatima ya Ujerumani mara hii na ile ya Spain na Holland keshokutwa. Mashabiki wa pweza huyu maarufu-mtabiri mpya wa dimba, wanadai "msiandikie mate na Paulo yupo."

Mwandishi: Martinez,Daniel (DW Lateinamerika)

Mtayarishi/Adapter: Ramadhan Ali

Uhariri: Miraji Othman