1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal asema hawawezi kuitambua Israel

22 Aprili 2008

-

https://p.dw.com/p/DlzS

DAMASCUS

Kiongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas anayeishi uhamishoni nchini Syria Khaled Meshaal amesema katu Hamas haliwezi kuitambua Israel.

Maneno hayo yanapingana na matamshi yaliyotolewa na rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter kufuatia mazungumzo yao nchini Syria mwishoni mwa wiki.Hapo jana Jimmy Carter alisema Hamas inajiandaa kukubali haki ya kuwepo kwa taifa la Israel na kusihi pamoja kama majirani kwa amani ikiwa kutakuwepo na makubaliano ambayo yataridhiwa na raia wote wa Palestina.

Kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal akizungumza huko Syria amesema wanachokitaka Hamas ni kuona Dola la wapalestina katika ardhi ya mashariki mwa Jerusalem,ukingo wa magharibi na Gaza ardhi ambayo Israel iliiteka katika vita vya mwaka 1967.Aidha kiongozi huyo amesisitiza kwamba lazima paweko Dola huru la Palestina ambalo mji mkuu wake utakuwa Jerusalem na bila ya kuwepo makaazi ya walowezi wa kiyahudi.Meshaal amesema hii haimaanishi kwamba watakuwa tayari kuitambua Israel pindi Palestina litakuwa dola huru bila ya kukaliwa na Israel bali watakuwa tayari kuacha matumizi ya nguvu ikiwa Israel itaondoka katika maeneo yote ya ardhi ya wapalestina.Marekani imesema matamshi hayo ya kiongozi wa Hamas hayajabadilisha lolote kuhusu msimamo wa kundi hilo kuelekea Israel.