1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong-II asemekana mgonjwa sana.

Abdulrahman, Mohamed10 Septemba 2008

Ashindwa kuhudhuria sherehe za miaka 60.

https://p.dw.com/p/FFKj
Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong II .Picha: dpa

Uvumi umezidi tangu Kim Jong-II aliposhindwa kuonekana jana katika sherehe hiyo ya miaka 60 ya taifa hilo, na hali hiyo imefuatia pia kutoonekana kwake hadharani kwa wiki kadhaa sasa, kukiwa pia na taarifa kwamba madaktari wa kigeni waliwasili Pyong Yang kumtibu. Baadhi ya ripoti zinasema madaktari hao ni kutoka China.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la Japan KYODO, viongozi wa Korea kaskazini wanakanusha kwamba Kiongozi wao mkuu Kim ni mgonjwa. Makamu wake katika safu ya uongozi aliye ana madaraka ya heshima Kim Yong Nam, amesema leo kwamba "kiongozi mkuu hana tatizo lolote" ,na afisa mmoja wa ngazi ya juu awa masuala ya diplomasia Song II Ho naye pia akakanusha ripoti juu ya hali mbaya ya afya ya Kim Jong II kuwa si kweli.

Ama kwa mujibu wa duru za Marekani na Korea kusini ni kuwa huenda Bw Kim mwenye umri wa miaka 66 amepata kiharusi pengine tangu wiki mbili zilizopita.

Afisa mmoja wa Korea kusini ambaye hakutaka kutajwa jina ,akizungumza na Shirika la habari YONHAP alitoa maelezo sawa na hayo akisema kiongozi wa korea kaskazini alifanyiwa upasuaji baada ya kupata kiharusi, lakini akatamka kwamba maisha yake hayako hatarini.

Kiongozi huyo amekua akisumbuliwa na kisukari na matatizo ya moyo na mara kwa mara kumekuweko na uvumi kuhusu hali ya afya yake.

Pamoja na kwamba wachambuzi wanaashiria hali yake ya sasa si kitisho kwa maisha yake, lakini ripoti zimetuwama katika suali ni kipi kitakachofuata.

Kim mtoto wa muasisi wa taifa hilo Kim Il Sung, alichukua madaraka ya uongozi wa taifa hilo baada ya kifo cha baba yake 1994.

Kile wadadisi na wachambuzi wanachokiona ni kuwa katika hali kama hiyo, maafisa wa chama tawala na viongozi wakuu jeshini watahiyari kuwa na mshikamano kunusuru utawala wao, kuliko kuzusha changa moto itakayosababisha kinyanganyiro cha kuwania madaraka.

Nafasi ya Kim Jong-II jana katika gwaride kubwa la kijeshi wakati wa sherehe hiyo ya miaka 60 ya taifa hilo, ilichukuliwa na Kim Yong-Nam , mzee wa miaka 80 na Rais wa baraza la uongozi la bunge la taifa Lakini haonekana kama mtu anayeweza kuchukua uongozi mkuu wa taifa hilo baada ya Kim, pindi ikilazimika.

Na ikiwa itatokea basi atakua ni kiongozi wa heshima tu na madaraka kuwa mikononi mwa mtu mwengine. Kwa sasa matukio katika taifa hilo pekee lilobakia lenye kufuata ukoministi kwa misingi ya kiongozi wa zamani wa iliokua Urusi Stalin aliyetawala kidikteta kuanzia 1924 hadi 1953 yanazidi kufuatiliwa na ulimwengu wa nje kwa karibu zaidi.