1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa kundi la waasi atangazwa kuwa waziri mkuu Ivory Coast.

27 Machi 2007

Kiongozi wa kundi la waasi New forces, Guillaume Soro,ametajwa kuwa waziri mkuu nchini Ivory coast baada ya kundi lake kutoa tangazo hilo kwenye tovuti yao.

https://p.dw.com/p/CHHS

kulingana na taarifa hiyo kwenye tovuti ya kundi la waasi wa New Forces,kiongozi wao Guillaime Soro ndiye waziri mkuu. Msemaji wa kundi hilo, Alain Lobognon alisema serikali na kundi hilo waliweka saini makubaliano hayo huko Ouagadougou mbele ya waziri wa usalama Djibril Bassole. Japo hapajakuwa na tangazo maalum,viongozi wamedokeza kuwa Soro atateuliwa.

Ikiwa tangazo hilo litatekelezwa na serikali ya Ivory Coast, hatua hii itakuwa ya kihistoria katika miaka sita ambapo Ivory Coast imekumbwa na mgogoro wa kisiasa, tangu kundi hilo la waasi,New Forces lilipoliteka eneo la kaskazini mwa nchi hiyo Septemba mwaka 2002. Soro amekuwa akiongoza asilimi 60 ya maeneo ya nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa kakao.

Guillaime Sorro mwenye miaka 34 alijaribu kuipindua serikali mwaka 2002,ambapo vita vya wenyewe kwa wenywe vilizuka na kusababisha mgawanyiko mkubwa baina ya serikali, makundi ya waasi na raia. Sorro anayehusika sana na harakati za mtazamo wa mrengo wa kushoto wa kijeshi, alikamatwa na polisi na kufungwa mara kadhaa kwa kuhusika na maandamano dhidi ya chama tawala nchini Ivory Coast.

Baada ya makubaliano ya kwanza ya amani mwaka 2003,Sorro aliteuliwa kuwa waziri wa habari hadi mwaka 2005. Na hadi mwaka huu Januari,ndipo kiongozi huyo wa kundi la waasi wa New Forces alipokubali tena kufanya mazungumzo na adui yake mkubwa rais Bagbo.

Na Mapema wiki hii Rais Laurent Gbagbo na Guillaime Soro,walitia saini makubaliano ya amani. Baadhi ya mapendekezo ya makubaliano hayo ni kuhusisha viongozi waasi kwenye serikali ya umoja ya Ivory Coast na serikali hiyo iunduwe katika wiki chache zijazo

Waziri mkuu wa sasa, Charles Konan Banny aliyeteuliwa na jamii ya kimataifa kwa madhumuni ya kuleta upatanishi alisema yuko tayari kujiuzulu ikiwa hatua hiyo itaokoa taifa la Ivory Coast.

Lakini utata mwengine uliopo ni kwamba hadi sasa waziri mkuu huyo hana uwezo mkubwa wa kisiasa kumshinda rais kama inavyotakikana,kwani Rais Gbagbo alikataa kumkabidhi madaraka waziri mkuu.

Na ikiwa Guillaume Soro atapwewa wadhifa huo, utata huo wa rais Gbagbo kutoa madaraka yake kwa waziri mkuu, ndio utakuwa kitendawili kingine kwa Ivory Coast. Kwani tangu jadi,viongozi hawa wawili wameshindwa kukubaliana na kutekeleza maazimio ya amani.

Isabella Mwagodi.