1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani Zimbabwe kung'atuka

Iddi Ssessanga
9 Januari 2018

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai amedokeza juu ya mabadililo ya kiuongozi katika chama chake, kufuatia kuondolewa mdarakani Robert Mugabe, na kusema sasa ni zamu ya vijana kushika uongozi.

https://p.dw.com/p/2qYfB
Simbabwe
Picha: DW/C. Mavhunga

Kiongozi huyo wa muda mrefu wa upinzani amekuwa akipambana na maradhi ya saratani. Tamko lake kwamba atajiuzulu linakuja wakati zimbabwe ikijiandaa kw auchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.

"Naangalia uwezekano wa sisi kizazi cha wazee kuachia hatamu za uongozi ili kuwapisha kizazi cha vijana kuendeleza jukumu kubwa tuliolianzisha pamoja miaka mingi iliyopita kwa baraka na msaada wetu kamili," alisema Tsvangirai, kiongozi wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) katika taarifa.

"Laazima tutambue umuhimu kwamba mikono mipya, ikiwa na baraka kamili za watu, inapaswa kuongoza  mapambano na kulipeleka taifa mbele."

Tsvangirai, mwenye umri wa miaka 65, alitangaza mwaka uliyopita kwamba anauguwa maradhi ya saratani ya utumbo na amekuwa akipatiwa matibabu katika nchi jirani ya Afrika Kusini.

Simbabwe Präsident Emmerson Mnangagwa besucht kranken Oppositionsführer Morgan Tsvangirai
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa (kulia) akimjulia hali Morgan Tsvangirai (katikati), anaeuguwa maradhi ya saratani ya utumbo.Picha: DW/P. Msvanhiri

Nelson Chemisa kumrithi Tsvangirai?

Waziri mkuu huyo wa zamani na kiongozi wa chama cha wafanyakazi, ametumia muda mwingi zaidi wa miongo miwili iliyopita kukijenga chama cha MDC ili kukifanya kuwa chama mbadala kwa chama tawala cha Mugabe, ZANU-PF.

"Binafsi nihisi kuridhika wakati nikiangalia safari kubwa tuliyotembea pamoja hata wakati huu ninapotafakari kuhusu wakati wa baadae," alisema Tsvangirai. Chama cha MDC kina makamo watatu wa rais: Thokozani Khupe, Elias Mudzuri na Nelson Chamisa.

Chamisa mwenye umri wa miaka 39, mbunge machachari na kiongozi wa upinzani bungeni, anapewa nafasi kubwa ya kuchukuwa uongozi wa chama. Tsvangirai aliitolewa serikali ya rai mpya Emmerson Mnangagwa kuendesha uchaguzi huru na wa haki, baadae mwaka huu.

Mnangagwa alichukuwa uongozi kutoka kwa Mugabe mwenye umri wa miaka 93, ambaye alijiuzulu Novemba 21, baada ya kuliongoza taifa hilo kwa miaka 37, baada ya kutupwa mkono na majenerali wake pamoja na chama chake.

"Utawala mpya unapaswa kueleza kwa ufasaha na kina, ratiba ya kuerejesha uhalali wa uongozi ambayo inahusisha utekelezaji wa mageuzi yanayohitajika kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na unaoaminika," alisema Tsvangirai.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.

Mhariri. Saumu Yusuf.