1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa waasi aunga mkono uchaguzi CAR

Mjahida 23 Desemba 2015

Kiongozi wa waasi katika Jamhuri ya Afrika ya kati ambaye mwezi huu alitangaza jimbo huru lililo chini ya uongozi wake, amesema ameacha kuupinga uchaguzi muhimu unaofanyika mwishoni mwa juma hili nchini humo.

https://p.dw.com/p/1HS9H
General Nouredim Adam
Picha: DW/S. Schlindwein

Noureddine Adam, anayekiongoza kikundi cha FPRC kilichokuwa muungano wa waasi wa Seleka ametajwa kama "Adui nambari moja" na serikali ambayo ilikuwa imeitisha kukamatwa kwake kufuatia jaribio lake la kupinga kufanyika kwa uchaguzi.

Tangazo hili limejiri baada ya mazungumzo ya siku kadhaa yaliofanyika katika nchi jirani ya Chad yaliyonuiwa kuondoa kikwazo kitakachokwamisha uchaguzi wa rais na bunge siku ya jumapili, uchaguzi unaoangaliwa kuwa muhimu katika kumaliza miaka kadhaa ya umwagikaji damu.

"Vuguvugu letu linaahidi kutoa mchango chanya na wa kweli ili uchaguzi ufanyike kwa utulivu, bila vurugu na utakaowashirikisha raia wengi," ilisema taarifa iliyotolewa na utawala wa Chad ulioshiriki mazungumzo hayo.

rais wa Zamani Francois Bozize
rais wa Zamani Francois BozizePicha: AFP/Getty Images

Noureddine Adam, alikuwa kamanda wa pili katika kundi la waasi wa kiislamu wa Seleka lililochukua madaraka mwanzoni mwa mwaka 2013 katika taifa hilo lililo na wakristo wengi, na kumuondoa madarakani rais wa wakati huo Francois Bozize.

Kampeni za uchaguzi zaanza

Kampeni za uchaguzi zilianza hapo jana huku wagombea wasiozidi 30 wakitarajiwa kugombea nafasi ya urais. Aidha Bozize, aliyeishi uhamishoni hasa nchini Uganda tangu alipotolewa madarakani, alinyimwa nafasi ya kugombea katika uchaguzi wa jumapili baada ya mahakama ya kikatiba kukataa ombi lake mapema mwezi huu.

Kando na hilo bado Bozize anaungwa mkono na raia wengi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati hasa katika eneo la Kusini Magharibi, siku ya Jumanne chama chake cha

Kwa Na Kwa (KNK) kilimuunga mkono mgombea aliye na miaka 58 Anicet-Georges Dologuele, hatua inayoonekana huenda ikatoa nafasi ya ushindi kwa mgombea huyo aliyekuwa Waziri Mkuu nchini humo.

Awali katibu Mkuu wa chama hicho cha KNK Bertin Bea alimwambia mgombea Anicet-Georges kwamba watafanya kila wawezalo kuhakikisha anashinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi, na kumhakikishia kuwa ana uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa chama hicho, wanaharakati na hata Francois Bozize."

Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wakishiriki kura ya maoni
Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wakishiriki kura ya maoniPicha: Getty Images/AFP/M. Longari

Mgombea mwengine katika uchaguzi huo ni Martin Ziguele, anayesemekana kupata uungwaji mkono kutoka koloni la zamani la nchi hiyo Ufaransa.

Wagombea wengine wanaoonekana kuwa na nafasi ya kuchukua ushindi ni Karim Meckassoua, na Xavier Sylvestre Yangongo, jenerali wa zamani ambaye mabango yake ya kampeni yanamtaja kama nguzo ya Jamhuri ya Afrika ya Kati. Iwapo hakutakuwa na mshindi wa moja kwa moja siku ya jumapili duru ya pili ya uchaguzi itafanyika tarehe 16 mwezi wa Januari.

Uchaguzi nchini humo umecheleweshwa kwa muda mrefu, kura ya maoni ambayo ni hatua ya kwanza ya kupisha uchaguzi wa rais na bunge kufanyika ili kuirejesha nchi katika utawala wa kidemokrasia kufuatia serikali mbili za mpito ilifanyika mnamo tarehe 13 mwezi huu wa Desemba.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/REUTERS

Mhariri: Iddi Ssessanga