1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan aunganisha nguvu na Marekani kusaida wakulima Afrika.

Mohamed Dahman12 Juni 2008

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ameelezea matumani yake kwa Afrika kuondokana na umaskini uliojikita barani humo.

https://p.dw.com/p/EIEg
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ambaye sasa ni kiongozi wa shirika la maendeleo ya kilimo AGRA.Picha: AP

Annan ameelezea matumaini yake hayo baada ya shirika la misaada analoliongoza kuunganisha nguvu zake na Marekani.

Makubaliano hayo ya ushirikiano yameunganisha mojawapo ya mashirika makubwa kabisa duniani ya kutowa ruzuku katika maendeleo ya kilimo barani Afrika ambayo yanalenga kuwasaidia wakulima wadogo wadogo kuongeza uzalishaji wao wa mazao.

Katika mahojiano baada ya kusaini mpango wa ushirikiano kwa niaba ya Muungano kwa ajili ya Mapinduzi ya Kilimo barani Afrika (AGRA) ambalo ni shirika la maendeleo ya kilimo na Shirika la Changamoto ya Milinia la serikali ya Marekani MCC Annan amesema shirika hilo la Marekani MCC linatowa kitu muhimu katika mkanganyiko wa kilimo barani Afrika ambao ni uwekezaji wa miundo mbinu.

Amesema katika mahojiano na shirika la habari la AFP kwenye makao makuu ya shirika hilo la Changamoto Moto ya Milinia MCC mjini Washington Marekani kwamba uwekezaji unaleta kitu muhimu ambacho kimekuwa kikikosekana katika kilimo cha Afrika na pia kinaelezea kushindwa kwa ulimnwegu mzima wa kilimo.

Makubaliano hayo yanakuja wakati bara hilo lililo maskini kabisa duniani likiyumba kutokana na mzozo wa chakula duniani uliosababishwa na kuongezeka kwa bei za nishati na zile za bidhaa za walaji.

Barani Afrika ambapo wakulima wadogo ndio wenye kuhodhi sekta ya kilimo Annan mweyekiti huyo wa shirika la AGRA amesema shirika lake linatowa mbegu,mbolea na mafunzo lakini mara tu pale wakulima wanapovuna mazao yao wanajikuta kuwa hawawezi kuyafikisha sokoni.

Kwa msaada wa shirika hilo la Marekani (MCC) la kupiga vita umaskini AGRA litakuwa linaweza kufunguwa baadhi ya barabaraba zinazounganisha mashamba ili kuweza kupata bidhaa zao kufika katika masoko.

Annan anaona msaada huo wa MCC utawapatia wakulima hao wa Afrika mabadiliko makubwa na kuwapatia mambo ambayo wamekuwa wakinyima kwa muda mrefu.

Annan mwanadiplomasia wa zamani wa Ghana mwenye umri wa miaka 70 ambaye ni Katibu Mkuu wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kutokea kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika kutumikia wadhifa huo kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2006 amesema italichukuwa shirika lake kupata ushindi wa uhakika kwa harakati zake katika kipindi kisichozidi miaka mitano na ushee ambapo watakuwa wameweza kuongeza maradufu au hata mara tatu uzalishaji wa chakula kwa baadhi ya nchi.

Ushirikiano huo mpya wa mashirika hayo kwanza utazingatia juhudi za Ghana, Madagascar na Mali.

Kwa mujibu wa Annan matumizi ya mbolea barani Afrika kwa kweli yako katika kiwango cha sifuri na kutokana na kupanda kwa bei za mbolea kunakosababishwa na kupanda kwa bei za nishati wakulima wanazidi kushindwa kumudu na inabidi watosheke na ardhi ya kilimo isiokuwa na rutuba kabisa.

Ametowa mfano mzuri wa majaribio ya harakati zao nchini Kenya ambapo shirika lake liliomba Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa kujiunga katika kutowa garantii au dhamana ya dola milioni tano kuiwezesha Benki ya Hisa nchini Kenya kuingiza nchini humo mbolea yenye thamani ya dola milioni 15 ambayo ilisambazwa nchini humo kwa msaada wa serikali.

Hayo yanaonekana kuwa makubaliano ya kwanza ya kifedha ya aina hiyo na pengine ndio makubwa kabisa kwa wakulima katika eneo hilo.

Hivi sasa benki nyengine zimeonyesha utashi wa kujiunga na mipango ya aina hiyo.

Annan anasema hatua moja muhimu kabisa itakayoweza kuchukuliwa na watu katika nchi zilizoendelea kusaidia kuitowa Afrika kwenye umaskini ni kuzishawishi serikali zao kuwa na biashara ya haki na ya wazi na kukamilishwa kwa mazungumzo ya kile kinachojulikana kama mazungumzo ya biashara duniani ya Duru ya Doha.