1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kisa cha kuteswa wanajeshi Coesfeld

Muno, Martin 13 Machi 2008

Korti kuu ya Münster yatoa hukmu kali dhidi ya kuteswa makruta wa kambi ya Coesfeld

https://p.dw.com/p/DNp9
Kambi ya kijeshi ya Freiherr-vom-Stein huko Coesfeld mjini MünsterPicha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha zaidi na hukmu ya kesi dhidi ya kudhalilishwa makruta wa jeshi la shirikisho Bundeswehr katika kambi ya COESFELD.


Walimu sita wa zamani wa Bundeswehr wamehukumiwa kwasababu wamewadhalilisha makruta katika kambi ya Coesfeld.Hukmu hiyo imesifiwa na wengi wa wahariri wa magazeti ya Ujerumani

Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linachambua.


"Bora.Hukmu ya kesi ya Coesfeld inadhihirisha mipaka waliyowekewa waalimu wa jeshi la shirikisho na viongozi wao.Haiwezi kua hata kidogo, kwamba mateso na madhila yawe sehemu ya mafunzo wanayopatiwa raia wanaovaa jozi za kijeshi-eti kwaajili ya kuwaandaa kushiriki katika opereshini za kulinda amani nchi za nje.Ni habari za kutia moyo kuona wamba wahalifu hivi sasa wamehukumiwa.Za kuvunja moyo lakini ni kwamba jeshi limeshindwa kuepusha kisa kama hicho kisitokee.Dalili zilianza kuchomoza tangu mwanzo ,kwamba jeshi la shirikisho Bundeswehr lina ila.Sasa cha kufanya ni kipi?Muhimu kwanza ni kuhakikisha kisa cha Coesfekld hakidharauliwi.Na wala watu wasijidai kuhoji eti visa kama hivyo haiviepukiki.Kambi za kijeshi sizigeuzwe kamwe mahala pa watu kuteswa na  kudhalilishwa.Wanajeshi wanastahiki mafunzo ya maana na sio kufundishwa ukatili ."


Gazeti la TAGESZEITUNG la mjini Berlin linaandika:


" Makruta wengi walipendezewa na mazowezi hayo.Licha ya kugiza jinsi watu wanavyonyoongwa,licha ya kujazwa maji kinywani na puwani-visa vinavyolingana na vile vinavyotumiwa sana na shirika la upelelezi la Marekani CIA, na licha ya wakuu waliokua wakijifanya kama "wasasi wakubwa wa wanyamapori:mwaka 2004 hakuna makruta yeyote wa kambi ya Coesfelder Freiherr -vom Stein aliyejaribu kusitisha mafunzo yake kabla ya wakati.Na hapo ndipo panapokutikana umuhimu wa hukmu ya kifungo na faini iliyopitishwa na korti kuu ya mjini Münster jana ,katika kesi kubwa kabisa ya uhalifu kuwahi kushuhudiwa katika historia ya jeshi la shirikisho Bundeswehr.Hukmu hiyo inamgutua kila afisa wa ngazi ya juu na wa ngazi ya chini pia kwamba mateso si sehemu hata kidogo ya mafunzo ya makruta na kwamba jeshi la shirikisho Bendeswehr si gengi la mamluki wasiokua na uadilifu wa aina yoyote ile."


Gazeti la Die Welt linajiuliza:


"Ndo kusema kambi ya kijeshi ya Coesfeld,katika eneo tulivu la Münster inakutikana karibu na jela ya Abu Gharaib ya Irak au vipi?Au zinalingana kutokana na visa vya udhalilifu?Suala hilo linajibiwa kwa namna tofauti,tangu msimu wa mapukutiko mwaka 2004,pale visa vya kuigiza utekaji nyara na kuhojiwa makruta vilipoanza kugonga vichwa vya habari humu nchini.Wakati ule ilitajwa kua wanajeshi wanaopatiwa mafunzo ya kimsingi wameteswa na kuadhibiwa kwa umeme.Lakini baadhi ya wanajeshi wamesema mahakamani mazowezi yalikua "yakuvutia kupita kiasi."


Na hatimae gazeti la FRANKFURTER ALGEMEINE ZEITUNG linaandika.


Kutokana na sababu za kihistoria,linapohusika  suala la haki za wanajeshi, jeshi la shirikisho Bundeswehr  linaangaliwa kua jeshi la kiraia linayoyapita mengine yote ulimwenguni.Hali hiyo lakini haibadilishi ule ukweli kwamba kazi ya mwanajeshi haiwezi kulinganishwa na kazi nyenginezo.Hatari na usumbufu unaotokana na kazi hiyo,wajerumani wameanza kuugundua ukweli huo tangu jeshi la shirikisho Bundeswehr lilipoanza kutumika nchi za nje,katika maeneo ambako hali ni ngumu kuliko katika vituo vya mazowezi.Visa kama hivi vya Coesfeld vinatokea lakini ni nadra.