1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kisa cha manuari ya mazoezi ya kijeshi Gorch Fock

24 Januari 2011

Waziri wa ulinzi wa serikali kuu Karl-Theodor zu Guttenberg atiwa kishindo kutokana na zoezi la nguvu lililosababisha kifo cha kadeta mmoja wa kike.Masuala kadhaa yanahitaji majibu wanasema wahariri.

https://p.dw.com/p/101Ze
Manuari ya Gorch Fock ya UjerumaniPicha: dapd

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha zaidi hii leo na kishindo kinachomkumba waziri wa ulinzi Karl-Theodor zu Guttenberg kufuatia kifo cha kadeti mmoja wa kike mwenye umri wa miaka 25 alipokuwa akifanya mazowezi katika manuari ya Gorch Fock.

Gazeti la Bild linasema waziri zu Guttenberg ameamuru uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu kisa hicho.Hata hivyo gazeti la "Ludwigsburger Kreiszeitung" linahisi waziri wa ulinzi anakumbwa na masuala chungu nzima .Gazeti linaendelea kuandika:

Kwanini palihitajika saa saba nzima hadi mamaake kadeti huyo alipoarifiwa kuhusu kifo cha binti yake?Imekwendaje hata muda mfupi baada ya tukio hilo watu wakawa wanasherehekea karnavali ndani ya meli?Na kwanini watu walilazimishwa kupanda mlingoti katika wakati ambapo muongozo unalitaja zoezi hilo kuwa ni la khiari?Bila shaka mafunzo ya makadeti si sawa na kituo cha kupawatia tiba na mazowezi wagonjwa .Lakini mazoezi yanapokiuka uwezo wa binaadam,inamaanisha kuna kasoro katika jeshi la shirikisho Bundeswehr.Waziri wa ulinzi atakuwa na kazi ya kujieleza mnamo siku na wiki zijazo.

Norbert Schatz
Kepteni Norbert SchatzPicha: picture alliance/dpa

Gazeti la Nürnberger Nachrichten linaandika:

Ni jambo la kustaajabisha kwamba waziri zu Guttenberg anampokonya cheo chake kepteni wa manuari hiyo hata kabla ya tume iliyochaguliwa kuanza kuchunguza yaliyotokea katika manuari hiyo.Na hali hiyo katika wakati ambao yeye mwenyewe zu Guttenberg daima amekuwa akikosoa dhana dhidi ya wanajeshi.Yadhihirika kana kwamba anatafutwa mkosa hapo.Hasa kwakua yasemekana,kepteni wa manuari hiyo amefukuzwa kutokana na ripoti za vyombo vya habari na sio kutokana na ripoti ya jeshi la shirikisho.Tutaraji tuu kwamba hapatahitajika miezi miwili na nusu hadi ripoti itakapochapishwa.

Deutschland Verteidigungsminister Karl-Theodor zu Guttenberg Pressekonferenz
Waziri wa ulinzi Karl-Theodor zu GuttenbergPicha: picture alliance/dpa

Na hatimae gazeti la Sächsische Zeitung linakumbusha kishindo kama hiki kilichowahi kumtikisa waziri wa ulinzi Karl -Theodor zu Guttenberg.Gazeti linaendeleav kuandika:

Masaa kadhaa kabla, uvumi kuanza kuzagaa kuhusu visa vya kuchusha na viofu vilivyotokea katika manuari ya mazoezi,zu Guttenberg alijitokeza hadharani kupinga dhana na kudai uchunguzi ufanywe.Lakini hata kabla ya uchunguzi kuanza,ripoti za magazeti zikazungumzia jinsi zu Guttenberg alivyobadilisha fikra yake kufumba na kufumbua.Mambo yalikuwa hivyo hivyo kisa cha Kundus kilipojiri.Wakati ule pia waziri wa ulinzi alikuwa mara anasema hivi na mara anasema vyengine.Wakulaumiwa walikuwa wengine kabisa.Walilazimika kuondoka,na nyota yake ikazidi kung'ara.Lakini mtindo wa kuwaachisha kazi maafisa,hata kama ni sawa,unaweza kumfujia kipenzi cha umma sifa zake miongoni mwa wanajeshi.Na wapinzani wake chungu nzima na marafiki wanaomhusudu,watajipatia fursa ya kumtia ila.

Mwandishi:Hamidou Oummil/Inlandspresse

Mpitiaji:Abdul-Rahman