1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wizara ya afya DRC yathibitisha kisa cha Ebola Kivu Kusini

Angela Mdungu
19 Agosti 2019

Wizara ya afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imethibitisha kisa kipya cha maambukizi ya Ebola katika wilaya ya Walikale inayodhibitiwa na kundi la waasi.

https://p.dw.com/p/3O8sv
Kongo Ein Kind bekommt eine Ebola-Impfung in Goma
Picha: Getty Images/AFP/A. Wamenya

Hayo yanajiri wakati idadi ya waliothibitika kuambukizwa maradhi hayo katika mkoa wa Kivu Kusini ikipanda na kuwa watu 30.Taarifa ya wizara ya afya nchini Kongo imesema maambukizi hayo ya hivi karibuni yamethibitishwa katika kijiji cha Pinga kilichoko umbali wa kilomita 150 Magharibi mwa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini ambao pia umekumbwa na maradhi ya Ebola. Ugonjwa huu ulianzia katika miji ya Beni na Butembo ambayo pia iko katika mkoa huo wa Kivu Kaskazini.

Katika taarifa yake iliyotolewa usiku wa kuamkia leo na kunukuliwa na shirika la habari la Reuters, wizara hiyo ya afya imethibitisha kuwa mtu wa tatu ameambukizwa ugonjwa huo hatari katika mkoa wa Kivu Kaskazini, masafa ya kilimita zipatazo 700 Kusini mwa kitovu cha mripuko huu unaoendelea Mashariki mwa Congo.

Mwandishi wa DW mjini Bukavu Mitima Delachance aliyesafiri na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Congo, MONUSCO uliokwenda leo katika kijiji cha Kilungutwe kwenye wilaya ya Mwega yalikoripotiwa maambukizi hayo katika mkoa wa Kivu Kusini, amesema waathirika hao watatu wote wameaga dunia.

Ingawa uelewa juu ya Ebola umeongezeka, na miundombinu ya kupambana nao imeboreka kuliko ilivyokuwa siku za nyuma, kupanuka kwa maeneo ya maambukizi yake hadi katika sehemu zilizo chini ya waasi, kunauzifanya juhudi za kuudhibiti kuwa ngumu zaidi, na kuzidisha hatari kusambaa haraka.

Karibu wilaya nzima ya Walikale inadhibitiwa na na kundi la mai mai, na limezungukwa na msitu mnene, na haifikiki kirahisi kwa sababu ya ubovu wa barabara.

Kuanzia mwaka jana, watu zaidi ya 1900 wamekwishafariki kutokana na ugonjwa wa Ebola, hiyo ikiwa idadi ya pili kwa ukubwa ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo, baada ya ile ya watu 11,300 waliokufa kutokana na ugonjwa huo Magharibi mwa Afrika, katika mripuko mbaya zaidi wa Ebola ulioanza mwaka 2014 na kuendelea hadi 2016.

Tangu wakati huo wataalamu wa tiba wamegundua dawa bora katika mapambano dhidi ya Ebola, zikiwemo  aina mbili ambazo hivi sasa zinatumiwa katika ngazi ya majaribio, na zimeweza kuponya zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa waliozitumia.

Lakini matumaini ya kuutokomeza ugonjwa huo yanakwamishwa na kukosekana kwa imani ya wananchi kwa huduma za afya kuhusiana na Ebola, na mabaki ya makundi ya waasi yanayoendelea kuisumbua nchi hiyo tangu miaka ya 1990.