1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha kuripuka tena vita Msumbiji

5 Aprili 2013

Mapigano kati ya wafuasi wa RENAMO na polisi yameangamiza maisha ya watu wanne na 13 kujeruhiwa katika mkoa wa kati wa Sofala.

https://p.dw.com/p/18APv
Mmojawapo wa majeruhi wa mapigano ya Muxungue huko SofalaPicha: Fernando Veloso

Nchini Msumbiji watu wanahofia hivi sasa baada ya miaka 20 ya amani,vita vya wenyewe kwa wenyewe visije vikaripuka upya kati ya waasi wa zamani wa RENAMO na serikali.

Hali imevurugika kufumba na kufumbua .Inatia wasi wasi na kuzusha hofu baada ya wanamgambo waliokuwa na silaha kutoka chama cha ukombozi wa taifa ,chama kikubwa cha upinzani nchini Msumbiji-RENAMO kuwashambulia wanajeshi wa kikosi cha kuingilia kati haraka-FIR katika mtaa wa Muxungué.

Kwa kufanya mashambulio hayo ,wafuasi wa RENAMO walitaka kulipiza kisasi dhidi ya polisi na pia kuwafungua wenzao waliowekwa korokoroni.Siku moja kabla ya hapo wanajeshi wa kikosi cha kuingilia kati haraka waliutawanya mkutano wa wafuasi wa RENAMO huko MUXUNGUÉ na kuwakamata wanachama 15 wa RENAMO.Kwa mujibu wa polisi wanachama hao walikuwa wakifanya mazoezi ya kijeshi.

Eti RENAMO wanaweza kweli kuanzisha vita?

Statue Samora Machel in Chimoio
Sanamu la rais wa kwanza wa Msumbiji Samora Machel huko ChimoioPicha: DW/Johannes Beck

Katika miji mengine pia mfano wa Gondola katika mkoa wa kati wa Manica,machafuko yamekuwa yakiripotiwa wiki na miezi iliyopita kati ya polisi na wafuasi wa RENAMO.Hali inatisha zaidi katika mkoa wa Sofala-ngome ya zamani ya RENAMO.Katika enzi za vita vya wenyewe kwa wenyewe,huko ndiko RENAMO walikokuwa na makao makuu yao katika mbuga ya wanyama ya Gorongosa,wenyewe wanayaita "Casa Banana."

October mwaka jana kiongozi wa RENAMO Afonso Dhlakama na wanachama kadhaa wengine wa chama hicho,walirejea katika kituo hicho cha zamani cha uongozi wa wanamgambo.Kwa kufanya hivyo alitaka kulalamika dhidi ya kutengwa RWNAMO na serikali inayoongozwa na chama cha FRELIMO.Kila mara amekuwa akitishia kurejea upya msituni na kuanzisha tena vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji.Sultan Musa ,mwakilishi wa wakfu wa Konrad Adenauer nchini Msumbiji anahisi kitisho cha kuripuka vita vya wenyewe kwa wenyewe kipo.Anahisi serikali haizingatii kwa makini mazungumzo pamoja na RENAMO.Na kuambatana na katiba na makubaliano ya amani ya Roma,serikali hailazimiki kufanya hivyo kwasababu mazungumzo yanabidi yafanyike bungeni..Ukweli lakini ni kwamba RENAMO haina nguvu bungeni kuweza kushawishi maamuzi na ndio maana wanashikilia kuzungumza na serikali."

Frelimo wamefaidika na makubaliano ya amani

Afonso Dlhkama, Präsident der RENAMO
Afonso Dhlakama, mwenyekiti wa chama cha upinzani cha RENAMOPicha: Ismael Miquidade

RENAMO wanaonyesha kukata tamaa.Wanamgambo hao wa zamani waliokuwa wakiangaliwa kama wenye kuelemea upande wa kambi ya magharibi,wameondoka patupu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipomalizika nchini humo.Walioibuka na ushindi ni FRELIMO waliokuwa wakielemea upande wa kambi ya mashariki.Wanafaidika pia na neema ya mali ghafi iliyogunduliwa nchini humo.

Mwandishi:Beck Johannes/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Josephat Charo