1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha kutoweka viumbehai Magazetini

Oumilkheir Hamidou
7 Mei 2019

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu kitisho cha kutoweka viumbe hai, uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump wa kutuma manuari za kivita Mashariki ya kati na mjadala kuhusu wake wenza na uraia wa Ujerumani magazetini

https://p.dw.com/p/3I48J
Frankreich l Weltkonferenz zur Artenvielfalt startet in Paris l Biene
Picha: picture alliance/dpa/N. Armer

Umoja wa mataifa umechapisha ripoti kuhusu viumbe hai ikimulika kitisho cha kutoweka aina fulani ya viumbe hai na mimea pamoja na madhara yake kwa binaadam. Wahariri takriban wa magezti yote ya humu nchini wamezungumzia kuhusu kitisho hicho. Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" linaandika:"Ripoti hiyo inakumbusha maradufu zile ripoti za baraza la mabadiliko ya tabianchi kuhusu kuzidi hali ya ujoto ulimwenguni. Mada hizo mbili sio tuu zina uwiano wa moja kwa moja-kwasababu kuzidi hali ya ujoto kunapalilia sio tuu kutoweka viumbe hai-bali pia madhara yake ni ya aina moja-yanatishia uhai wa viumbe na kuhimiza hatua kali zichukuliwe.

Maisha yatakuwa ya aina gani bila ya milio ya ndege misituni na bustanini?

Mhariri wa gazeti la Oldenburg,"Nordwest-Zeitung" anakwenda mbali zaidi anapoonyesha jinsi ulimwengu utakavyojiinamia bila ya viumbe hai. Gazeti linaandika:"Wazo la kutisha la kimya cha maumbile! "Husikii tena sauti za ndege misituni, wala bustanini! Ili kuepusha balaa hilo lililoashiriwa na wachunguzi, kuna kinachobidi kubadilika-kila mmoja wetu, kila kampuni na kila nchi. Mataifa ya viwanda na makampuni makubwa makubwa wamenyamaza kimya kwa muda mrefu lililpohusika suala la kuyahifadhi maumbile kwa na maendeleo endelevu. Lakini sasa wanaanza na wao pia kugutuka na kutishika na kugundua pia madhara yatakuwa makubwa."

Rais wa Marekani Donald Trump awashinikiza viongozi wa Iran

Rais wa Marekani Donald Trump anaendelea kupalilia makali ya mvutano pamoja na Iran. Ameamua kutuma manuari ya kivita katika eneo la mashariki ya kati. Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linaandika:"Kwa kutuma manuari iliyosheheni ndege za kivita na nyengine ya mabomu, rais Donald Trump anataka kuzidi kuchochea mvutano. Ndo kusema anapanga hivi karibuni kuhujumu kwa mabomu mji mkuu wa Iran Teheran, ikiwa mamullah wataiga anachofanya Trump na kutangaza kujitoa katika makubaliano ya mradi wa nuklea? Washirikia wake barani Ulaya wanabidi wabadilishe msimamo wao wa  kukaa kimya katika hali kama hii inayotisha.

 Uraia wa Ujerumani si kwa wake wenza

Mada yetu ya mwisho magazetini inamulika mjadala uliohanikiza kama uraia wa Ujerumani wapatiwe wake wenza wote, kama mhusika ameowa zaidi ya mke mmoja. Gazeti la "Passauer Neue Presse" linaandika:"Kila jamii yenye utamaduni na mila zake ina miko yake pia na ambayo haistahiki kuvunjwa. Katika nchi za magharibi zinazofuata imani ya kikristo, miko hiyo ni pamoja na ndowa ya wake wengi. Anaetaka uraia wa nchi hii, hawezi wakati huo huo kuowa zaidi ya mke mmoja. Kwa hivyo ni jambo la kusifiwa kwamba waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer haregezi kamba na anapanga kuwasilishwa mswaada ziada wa sheria kushadidia  hilo katika sheria ya kuomba uraia nchini Ujerumani.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresase

Mhariri: Josephat Charo