1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Klabu tatu za Ujerumani zaingia robo finali ya vikombe vya Ulaya

15 Machi 2007

baada ya bayern munich kukata tikjeti yake ya robo-finali ya champions League, jana Bayer Leverkusen na W.Bremen zilijitosa nazo katika hatua hiyo ya kombe la UEFA.

https://p.dw.com/p/CHcW
Wachezaji wa Bayern Leverkusen
Wachezaji wa Bayern LeverkusenPicha: AP

Baada ya changamoto za jana za Kombe la Ulaya la UEFA ,timu 3 za Ujerumani zimeingia katika robo-finali ya vikombe vya Ulaya:mabingwa Bayern munich katika champions League,Bremen na Leverkusen katika kombe la UEFA.

Bayern Leverkusen iliikomea jana RC Lens ya Ufaransa mabao 3-0 na kukata tiketi yake ya robo-finali ya kombe la UEFA.Bernd Schneider,mchezaji wa kiungo wa timu ya taifa, ndie alietamba kati ya uwanja upande wa Leverkusen.Mbali na Schneider muukraine Veroni, na mbrazil Juan, waliufumania mlango wa RC Lens kwa mabao.

Kocha wa Bayern Leverkusen, Michael Skibbe alitoa pongezi nyingi kwa timu yake jinsi ilivyotamba.

“shukurani nyingi kwa mchezo maridadi wa timu yangu leo hii.Timu imecheza kimkakati kabisa,imeweza kupata nafasi nyingi za kutia magoli na ilitamba kimchezo.Ilikua mechi nzuri sana ya kombe la UEFA.”

Nae mkurugenzi wa spoti wa Bayer Leverkusen,Rudi Völler alikuwa na haya ya kusema baada ya changamoto ya jana usiku:

“Ni barabara kuona Ujerumani ina timu 3 katika robo-finali ya vikombe vya Ulaya na si mbaya wakati huu kwa dimba la Ujerumani.”

Asema Rudi Völler,kocha wa zamani wa taifa.

Klabu ya pili ya ujerumani iliotamba jana ni Werder Bremen ilioamka hasa usingizini baada ya kipindi cha mapumziko.Almeida na Fritz Schindler ndio waliotia mabao ya Bremen katika lango la Celta Vigo.

Bayern Munich ilikwishakata tiketi yake ya robo-finali ya champions League baada ya wiki iliopita kuitimua Real Madrid ya Spian na hivyo imekuwa klabu ya tatu ya Ujerumani kuingia duru hiyo ya vikombe vya ulaya msimu huu.

Na taarifa za hivi punde kutoka Munich zasema kocha wao alieitwa karibuni kuokoa jahazi kwenda mrama,Ottmar Hitzfeld atabakia kuwa kocha alao kwa msimu mwengine ujao.Hitzfeld ndie alieiongoza Munich kutwa kombe la ulaya 2001 kabla kuiacha mkono baadae.Aliitwa majuzi tu kuikoa Munich baadaya kutimuliwa kocha Felix Magath.

Stadi wa zamani wa Munich Michael Ballack amependekeza munich ingekuwa bora kumchukua staid wao wa zamani Stefan effenberg kuwa kocha wao mpya.

Katika kombe la dunia la cricket huko Caribbean, Ireland ina miadi leo na Zimbabwe huko jamiaca. katika kundi D wakati Bermuda inaumana na sri Lanka katika kundi B.Sri Lanka mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu kutwaa ubingwa inaingia uwanjani mara ya kwanza leo ikicheza na Bermuda huko Trinidad