1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la afrika:

22 Januari 2008

Mabingwa Misri wanaonana leo na simba wa nyika Kameroun.nani atatamba ?

https://p.dw.com/p/Cw4q

Mali,Morocco na Tembo wa ivory Coast jana walifuata nyayo ya Ghana kwa ushindi katika dimba lao la ufunguzi la Africa cup.

Jioni hii,ni zamu ya wababe wengine 2 wa dimba la Afrika huko Kumasi, kupimana nguvu:mabingwa watetezi Misri na mahasimu wao simba wa nyika Kamerun. Baada ya kumuona Machael Essien jumapili, Didier Drogba na Solomon Kalou jana wakitamba na timu zao, leo ni zamu ya jogoo mwengine wa Afrika-Samuel Eto’o akiongoza hujuma za Kamerun katika lango la mabingwa Misri.

Baada ya timu hizo mbili kuondoka leo uwanjani, itakua zamu ya mabingwa wa afrika mashariki na kati-Sudan kukwepa risasi kali za Chipolopolo-Zambia.huu ni mpambano pekee kati ya CECAFA na COSAFA-mashirikisho ya kanda hizo mbili.

Simba wa nyika Kamerun wana kibarua kigumu hivi punde watakapoingia uwanjani mjini Kumasi kujaribu kuwavua taji mafirauni wa Misri.Changamoto hii ya leo itaamua nani mwishoe, ataparamia kileleni mwa kundi hili.Zaidi tutajua iwapo mabingwa Misri,bado wako kitini au tayari wamelinyanyua taji kichwani tayari kulivua.

Misri nma kameroun zina uhasama wa kale na sio tu Misri iliitoa Kamerun katika nusu-finali ya kombe lililopita nyumbani,bali pia zilicheza finali ya 1986.

Wakati Samuel Eto’o –anaongoza hujuma za simba wa nyika leo, kumekuwa na wasi wasi iwapo mshambulizi wa Misri,Mohamed Aboutrika atashuka uwanjani kwani akiugua homa ya mafua.Aboutrika, alikua ufunguo katika kile kikosi kilichowatimua nje Tembo wa ivory Coast na kutwa ubingwa 2006 nyumbani Cairo.

Isitoshe, Misri haitacheza na stadi wa Middlesbrough ya Uingereza, Ahmed Hossam (mido),Mohammed Barakat na Hossam Ghali.Nahodha wa mafirauni hawa wa dimba Ahmed Hassan pia anaukosa mpambano huu jioni ya leo ,kwani amefungiwa miezi 3 kucheza dimba kwa kumhujumu adui kwa viatu pale Misri ilipotoka sare 0:0 na Burundi septemba mwaka jana.

Baada ya simba wa nyika na Misri kuondoka uwanjani leo, itakua zamu ya mabingwa wa afrika mashariki na kati-Sudan kupepea bendera ya CECAFA katzika kombe hili la Afrika kwa mchuano na Chipolopolo-Zambia.hii ni changamoto kati ya CECAFA na COSAFA katika medani ya CAF-shirikisho la dimba la Afrika. Sudan –muasisi wa kombe la afrika 1957 nyumbani pamoja na Misri .Ethiopia na Afrika Kusini, ililitwaa kombe la afrika 1970.Ikachukua miaka 32 kabla sasa kurudi katika finali hizi.Kwahivyo, matumaini sio tu makubwa mjini Khartoum na Omduraman,nyum,bani mwa klabu 2 zilizochangia wachezaji wake El Mirreikh na Al Hilal, bali katika kanda nzima ya Afrika mashariki na kati.

Chipolopolo –Zambia,zamani ikitamba na akina Kalusha Bwalya katika Kombe la Afrika.Ilicheza finali na Zaire iliorudiwa mara 2 1974 kabla chui kuja Ujerumani kwa kombe la dunia.

Zambia ni timu ya kutegemea na risasi za chipolopolo zaweza jioni hii zikaumiza Sudan.

Jana ,stadi wa Chelsea sio Didier Drogba,bali Salomon kalou ambae wadachi walimktalia uraia,ndie alielifumania lango la Super eagles Nigeria,na kutoroka na pointi 3 huko sekondi.Freddie Kanoute nae akautikisa wavu wa Benin kunyakua pointi 3 kwa Mali kabla wamorocco kuwadhibu chipukizi wa Namibia kwa mabao 5-1.